WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wahandisi Washauri nchini kutotumia vibaya vyeo na dhamana walizonazo kwa kuwalazimisha wakandarasi kununua bidhaa sehemu wanazotaka wao na badala yake wawashauri kununua bidhaa bora.
Pia
amewataka watendaji wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wakurugenzi wa
Halmashauri na Majiji nchini pamoja na Wahandisi Washauri kutumia
mabomba yanayozalishwa na viwanda vya ndani kwa kuwa yanakidhi viwango
vya ubora.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumamosi,
Desemba 3, 2016) wakati wa uzindizi wa kiwanda cha kutengeneza bidhaa
za plastiki cha Lodhia, akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya
kikazi mkoani Arusha.
“Serikali
inalenga kumaliza tatizo la ajira hasa kwa vijana na Serikali pekee
haiwezi kuwaajiri watu wote. Viwanda pekee ndivyo vyenye uwezo wa
kuzalisha ajira nyingi. Jukumu letu ni kuviunga mkono,” alisema.
Alisema
haoni sababu ya halmashauri na wakandarasi kununua mabomba kutoka nje
ya Arusha au nje ya nchi wakati bidhaa hizo zinazalishwa na wawekezaji
ndani ya mkoa huo na zinakidhi viwango vya ubora.
Hata hivto Waziri Mkuu aliwataka
watumishi wa kiwanda hicho kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa
ili kukiwezesha kuzalisha bidhaa nyingi zaidi na hatimaye kuongeza
ajira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Sailesh Pandit alisema
moja ya changamoto kubwa inayowakabili kiwandani hapo ni kushindwa
kuuza bidhaa wanazozalisha katika miradi mikubwa ya maji iliyotekelezwa
Mkoani Arusha.
Alisema
“licha ya kuwa na viwango vya ubora vilivyothibitishwa na Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) na ISO tunashindwa kuuza kutokana na hujuma
tunazofanyiwa na baadhi ya wahandisi wa Halmashauri na washauri elekezi
wa miradi ya maji mkoani hapa,”.
Mkurugenzi
huyo alisema "Mheshimiwa Waziri Mkuu mara kadhaa wakandarasi wamezuiwa
kununua mabomba ya maji kutoka kwenye kampuni yetu na badala yake
hulazimishwa kununua mabomba kutoka nje ya Mkoa wa Arusha na
kuisababishia serikali gharama zisizo za lazima "
Alisema
kampuni hiyo imetoa ajira rasmi kwa Watanzania 1,300 huku wengine zaidi
ya 500 wakinufaika kutokana na ushiriki wao katika utoaji wa huduma
kiwandani hapo. Kiwanda kinalipa wastani wa sh. bilioni 20 kwa mwaka
kama kodi na tozo mbalimbali.
Baada
ya kutoka kiwandani hapo Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha
kutengeneza bodi za magari cha Hanspaul ambapo amewataka Wakurugenzi wa
halmashauro zote nchini wanaohitaji magari ya kuzolea taka kwenda
kununua katika kiwanda hicho.
“Tumekua
tunanunua magari ya kuzolea taka kwa gharama kubwa ambayo ni kati ya
sh. milioni 300 hadi sh. milioni 400 kutoka nje ya nchi wakati magari
hayo yanapatikana Tanzania tena mkoani Arusha kwa sh. milioni 200,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Sign up here with your email