WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali inahitaji ushirikiano mkubwa na wafanyabiashara, hivyo
haitakubaliana na mtumishi yeyote wa umma atakayefanya urasimu kwa lengo
la kukwamisha uboreshaji wa sekta binafsi.
Amesema miongoni mwa maboresho
yanayofanywa na Serikali katika sekta binafsi ni pamoja na kuimarisha
utendaji wa watumishi na kuondoa urasimu katika utendajikazi wa kila
siku baada ya eneo hilo limelalamikiwa sana.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo
jana jioni (Ijumaa, Desemba 2, 2016) wakati akizungumza na
wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda mkoani Arusha kwenye Ukumbi wa
Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) akiwa katika siku ya kwanza ya
ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Ziara hiyo inalenga kuangalia
utelelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,Utendaji wa Serikali, kusikiliza
na kujionea kero zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo na kushirikiana
na viongozi wa Mkoa ili kuweza kuzipatia suluhisho.
“Serikali inafanya jitihada kubwa
katika kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kukuza
uchumi wa nchi yetu. Pia mapambano dhidi ya rushwa yanayofanyika ndani
ya Serikali na nje yanalenga kuleta maboresho makubwa katika sekta
binafsi ,” alisema.
Alisema Serikali inawataka
watendaji wake wote watumie lugha nzuri na rafiki katika kutoa huduma
kwa wafanyabiashara na wananchi kwa jumla na haitamvumilia mtumishi
yeyote atakayefanya urasimu ili mfanyabiashara atoe rushwa.
“Hatuwezi kuzungumzia maendeleo
katika sekta za maji, madini na viwanda bila ya kutaja wafanyabiashara
kwa sababu hata viwanda wao ndiyo wamiliki. Wafanyabiashara wameondoa
vijana wengi waliokuwa wanakaa vijiweni na kujadili mambo yasiyokuwa na
tija na kuwaajiri kwenye viwanda vyao,” alisema.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
amesema Serikali itaimarisha mipaka yake na kuzuia uingizwaji holela wa
bidhaa kutoka nje ambazo nyingi zinazalishwa hapa nchini huku lengo
likiwa ni kulinda viwanda vya ndani.
“Hatuwezi kuwalinda wazalishaji
wetu wa ndani bila ya kuweka doria ya nguvu kwenye mipaka yetu ili
kudhibiti uingizwaji wa bidhaa, hususan zinazozalishwa nchini. Lazima
Serikali isaidie kulinda masoko ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda
vyetu,” alisema.
Aliongeza kuwa “Mfano Jiji la
Arusha linajenga mradi wa maji na kisha mzabuni anaagiza mabomba kutoka
nje wakati viwanda vya ndani vinatengeza kwa viwango sawa au bora zaidi
ya yanayoagizwa nje, huko si kutaka kuongeza gharama ya mradi”? Alihoji.
Alisema Serikali haitakubali
kuruhusu viwanda vya ndani vife kwa kukosa soko baada ya uingizwaji wa
bidhaa za nje. “Ni lazima mitaji ya wafanyabiashara iheshimiwe na
ilindwe ili iweze kuleta tija inayokusudiwa,”.
Waziri Mkuu alisema Serikali na
sekta binafsi zimefanya jitihada kubwa katika kuhakikisha kunakuwa na
uwekezaji kwenye sekta ya viwanda nchini. Na sekta hiyo ndiyo
inategemewa katika kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa kati.
Kwa upande wao wafanyabiasha
wengi walilalamikia kuwepo kwa wingi wa kodi ambapo wameiomba Serikali
kuangalia uwezekano wa kuzipunguza ili kuwaondolea usumbufu.
Sign up here with your email