Mechi
14 za Ligi Kuu ya Vodacom zinatarajiwa kufanyika wakati huu wa msimu wa
kufunga mwaka 2016 na mbili za zitafungua mwaka 2017 ambako Kituo cha
Televisheni cha Azam – Wadhamini wenza wa ligi hiyo, wamethibitishia
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupata burudani kwa michezo
yote kulingana na ratiba.
Katika Ligi hiyo ambayo pia
inabarikiwa na Benki ya Diamond Trust (DTB), michezo 15 ya kipindi cha
sikukuu za kufunga na kufungua mwaka inatarajiwa kuanza saa 10.00 jioni
isipokuwa ule wa Mbao FC na Mwadui uliopangwa kuanza saa 8.00 mchana
kama itakavyojieleza hapo chini kwenye mtiririko wa ratiba.
Burudani kwa Wote katika michezo
hiyo kutoka Azam Tv, zinaanzia mchezo wa kesho Ijumaa wa Desemba 23,
mwaka huu ulipewa jina la Na. 129 utakaozikutanisha timu za African Lyon
na Young Africans kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Kamishna wa
mchezo anatarajiwa kuwa Idelfonce Magali kutoka Morogoro.
Katika mchezo huo unaotarajiwa
kuchezeshwa na Mwamuzi, Ludovic Charles kutoka mkoani Tabora akisaidiwa
na John Kanyenye wa Mbeya (Mshika Kibendera Na. 1) na Alnord Bugado wa
Singida (Mshika Kibendera Na. 2), Mwamuzi wa Akiba – Mezani anatarajiwa
kuwa Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam.
Jumamosi Desemba 24, 2016
kutakuwa na mechi sita ukianzia ule wa Mbeya City na Toto Africans
zitacheza kwenye Uwanja wa Sokoine jijiji Mbeya katika mchezo Na. 130
utakaosimamiwa na Kamishna George Komba wa Dodoma wakati Mwamzi wa kati
atakuwa Shakaile ole Shangalai wa Pwani huku wasaidizi wake wakiwa ni
Khalfan Sika pia wa Pwani na Vecent Milabu wa Morogoro. Mwamuzi wa akiba
atakuwa Cherles Mwamlima.
Mchezo Na. 131 utazikutanisha
timu za Kagera Sugar na Stand United katika Uwanja wa Kaitaba, uliko
Kagera ambako utasimamiwa na Kamishna Nassoroi Hamduni wa Kigoma huku
Mwamuzi akiwa ni Jacob Adongo wa Mara akisaidiwa na Joseph Masija na
Robert Luhemeja kutoka Mwanza na Mezani atakuwa Jonesia Rukyaa wa
Kagera.
Ndanda itaendelea kubaki nyumbani
kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara na baada ya kucheza na Simba
juma lililopita na kupoteza mchezo huo, safari hii inaikaribisha Mtibwa
Sugar ya Morogoro katika mchezo Na. 132 utakaosimamiwa na Kamishna
Jimmy Lengwe wa Morogoro wakati Mwamuzi atakuwa Andrew Shamba wa Pwani
akisaidiwa na Haji Mwalukuta wa Tanga na Jeremiah Simon wa Dar es
Salaam. Mezani atakuwa Abubakar Mtulo.
Siku hiyo pia kutakuwa na mchezo
kati ya Simba na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Mchezo
huo Na. 133 utafanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambako utasimamiwa
na Tito Haule wa Morogoro na kuchezeshwa na Mwamuzi Hans Mabena wa
Tanga. Mabena atasaidiwa na Omari Kambangwa wa Dar es Salaam na Khalfan
Sika wa Pwani wakati Mbaraka Rashid wa Dar es Salaam atakuwa Mwamuzi wa
Akiba – mezani.
Baada ya kulala Mbeya mbele ya
Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Majimaji ya Songea itakuwa
mwenyeji wa Azam FC ya Dar es Salaam ambayo juma lililopita iliambulia
sare tasa kutoka kwa African Lyon. Majimaji na Azam zinakutana kwenye
mchezo Na. 134 utakaofanyika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Katika mchezo huo ambao Mwamuzi
atakuwa Ngole Mwangole wa Mbeya ambaye ni mwamuzi bora wa Ligi Kuu ya
Vodacom msimu uliopita, atasaidiwa na Mirambo Tshikungu na Mashaka
Mwandembwa – pia wote wa Mbeya huku kamishna akiwa ni David Lugenge wa
Iringa.
Mwadui ambayo ilianza vibaya duru
la pili kwa kupoteza mchezo uliopita, Jumamosi Desemba 24, mwaka huu
itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mwadui Complex
mkoani Shinyanga. Mchezo huo Na. 135, utasimamiwa na Kamishna Staricko
Nyikwa wa Singida katika mchezo utakaoanza saa 8.00 mchana ili kutoa
fursa kwa mdhamini Azam kuonesha mchezo huo moja kwa moja ikiwa na maana
ya mubashara.
Waamuzi wataongozwa na Emmanuel
Mwandembwa atakayesimama katikati kupuliza filimbi huku akisaidiwa na
Abdallah Uhako na Agnes Pantaleo wote wa Arusha na mezani anatarajiwa
kuwa Ezekiel Mboi wa Shinyanga.
Krismas, yaani Desemba 25, 2016
hakutakuwa na mchezo ila siku inayofuata Desemba 26, mwaka huu Ruvu
Shooting itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa
Mabatini, ulioko Mlandizi mkoani Pwani katika mchezo Na 136.
Manyama Bwire wa Dar es Salaam
atakuwa Kamishna wa mchezo huo wakati Mwamuzi ni Forentina Zabron wa
Dodoma akisaidiwa na Hassan Zani wa Arusha na Silvester Mwanga wa
Kilimanjaro. Mwamuzi wa akiba – Mezani atakuwa Andrew Shamba wa Pwani.
Desemba 28, mwaka huu kutakuwa na
mechi mbili ambako Young Africans ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa
Ndanda ya Mtwara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini katika mchezo Na. 137
ambako Juma Chiponda wa Tanga atakuwa kamishna wa mchezo huo.
Mwamuzi wa kati katika mchezo huo
atakuwa Eric Onoca wa Arusha akisaidiwa na Michael Mkongwa wa Njombe na
Janeth Balama wa Iringa. Mwamuzi wa akiba atakayekaa mezani atakuwa
Mwanahamisi Matiku wa Dar es Salaam.
Kadhalika siku hiyo, Majimaji ya
Songea itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa
Manungu ulioko Mvomero katika mchezo Na. 138 utakaosimamiwa na Kamishna
Pius Mashera wa Dodoma, utachezeshwa na Mathew Akrama kutoka Mwanza
akisaidiwa na Abdallah Rashid wa Pwani na Gasper Ketto wa Arusha.
Mwamuzi wa akiba atakuwa Selemani Kinugani.
Kadhalika Desemba 29, mwaka huu
kutakuwa na mechi mbili. Ruvu Shooting ya Pwani inatarajiwa kuwa
mwenyeji wa Simba ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam
katika mchezo ambao mwamuzi atakuwa Alex Mahagi wa Mwanza.
Katika mchezo huo Na. 139, Mahagi
atasaidiwa na Ferdinand Chacha pia wa Mwanza na Rashid Zongo wa Iringa
huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Hellen Mduma wa Dar es Salaam. Kamishna
wa mchezo atakuwa Peter Temu wa Arusha.
Azam ya Dar es Salaam itatulia
nyumbani Uwanja wa Azam huko Chamazi ikicheza na Tanzania Prisons ya
Mbeya katika mchezo Na. 140 utakaosimamiwa na Elizabeth Kalinga wa Mbeya
huku Mwamuzi akiwa ni Jimmy Fanuel wa Shinyanga huku wasaidizi wake
wakiwa ni Makame Mdog pia wa Shinyanga na Abdallah Mkomwa wa Pwani huku
Kassim Mpinga akiwa ni mwamuzi wa akiba.
Saa kadhaa kabla ya kuingia mwaka
2017, yaani Desemba 31, mwaka huu kutakuwa na michezo miwili ambako
Mwadui ya Shinyanga itacheza na Kagera Sugar ya Kagera kwenye Uwanja wa
Mwadui mkoani Shinyanga katika mchezo Na. 141.
Kamishna anatarajiwa kuwa Nassib
Mabrouk wa Mwanza na Mwamuzi ni Isihaka Mwalile na wasaidizi wake ni
Hellen Mduma na Omary Kambangwa – wote kutoka Dar es Salaam. Julius
Kasitu wa Shinyanga anatarajiwa kuwa Mwamuzi wa Akiba.
Kadhalika siku ya funga mwaka,
Mbeya City inatarajiwa kucheza na Mbao FC kwenye Uwanja wa Sokoine
jijini Mbeya katika Mchezo Na. 143 ambao msimamizi wa mchezo atakuwa
Joseph Mapunda wa Ruvuma.
Mwamuzi katika mechi hiyo
anatarajiwa kuwa Hussein Athuman wa Katavi wakati wasaidizi wake
watakuwa ni Lulu Mushi wa Dar es Salaam na Nicholaus Makaranga wa
Morogoro. Mwamuzi wa Akiba Mezani atakuwa Mashaka Mwandembwa wa Mbeya.
Januari mosi kutakuwa na michezo
miwili tu ya kukaribisha Mwaka Mpya ambako Toto African ya Mwanza
itacheza na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba
katika mchezo Na. 144 utakaosimamiwa na Jovin Bagenda wa Kagera. Mwamuzi
atakuwa Israel Nkongo sambamba na wasaidizi wake Soud Lila na Frank
Komba, wote wa Dar es Salaam. Mwamuzi wa akiba mezani atakuwa Mathew
Akrama wa Mwanza.
Pia African Lyon ya Dar es Salaam
itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu katika mchezo Na. 142 utakaofanyika Uwanja
wa Uhuru, Dar es Salaam. Kamishna atakuwa Hamisi Kitila wa Singida
wakati Mwamuzi anatarajiwa kuwa Selemani Kinugani wa Morogoro wakati
wasaidizi wake ni Omary Juma wa Dodoma na Agnes Pantaleo wa Arusha
wakati mezani atakuwa Shafii Mohammed wa Dar es Salaam.
Mara baada ya michezo hiyo, Ligi
Kuu ya Vodacom itasimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la
Mapinduzi inayotarajiwa kuanza Januari mosi, mwaka huu.
Sign up here with your email