Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 05 Desemba, 2016
amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika wa Kampuni ya
utengenezaji wa ndege ya Boeing yenye makao yake nchini Marekani Bw. Jim Deboo ikiwa
ni sehemu ya juhudi za Serikali za kununua ndege kubwa kutoka kampuni hiyo.
Mazungumzo hayo
yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Uchukuzi
Dkt. Leonard Chamriho na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto
James.
Baada ya
Mazungumzo hayo Rais Magufuli amesema Serikali yake ya Awamu ya Tano
imedhamiria kununua ndege nyingine nne zikiwemo ndege kubwa 3 ambazo zitasaidia
kuinua uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja hapa nchini moja kwa moja
kutoka nchi zao.
"Sisi hapa
tunazungumza kuwa watalii hawajafika hata milioni 2 kwa mwaka, lakini nchi kama
Morocco inapata watalii zaidi ya milioni 12 kwa mwaka, hii yote ni kwa sababu
hatuna mashirika ya ndege ya kwetu, watalii wakitaka kuja hapa ni lazima waje
kwa kuungaunga, wafikie nchi nyingine halafu ndipo wapate moyo wa kuja huku,
licha ya kwamba sisi Tanzania ni miongoni mwa nchi 5 duniani zenye maeneo
mazuri yenye utalii.
"Kwa hiyo
niwaombe tu Watanzania wapende mali zao, kwa sababu wakati mwingine nikiangalia
mitandao na magazeti ni ajabu huwezi kuamini kama hao ni Watanzania, unakuta
wanasifia tu ndege za watu wengine na
wanazibeza za kwao" amesisitiza Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli
ametaja aina ya ndege mpya ambazo Serikali itazinunua kuwa ni ndege 1 aina
Bombardier Q400 Dash 8 NextGen
inayotarajiwa kufika nchini Mwezi Juni 2017, ndege 2 aina ya Bombardier CS300
zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili
nchini kati ya Mei na Juni, 2018 na ndege moja aina ya Boeing 787 Dash 8 Dream
Liner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 na inayotarajiwa kuwasili nchini Juni,
2018. Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika.
Dkt. Magufuli
amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi za Serikali zenye lengo la kuinua
utalii na kuimarisha uchumi wa nchi.
"Tumeleta
ndege aina ya Bombardier hapa, zimepunguza gharama za safari mfano kutoka Dar
es Salaam hadi Mwanza, sasa wanalipa kati ya 160,000/ hadi 200,000/- wakati
nauli ilishafika Shilingi laki 8 na kitu, lakini watu wengine utakuta wanazungumzazungumza
wee maneno ya hovyo kwa kutumiwa, tumeshaamua na tutafanya hivyo"
amesisitiza Rais Magufuli.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli ameagana na aliyekuwa Mwakilishi
Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika hapa nchini (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero
ambaye amepandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) Ukanda wa Kusini mwa Afrika katika ofisi zake zilizopo Afrika
Kusini.
Rais Magufuli
amemshukuru Dkt. Tonia Kandiero kwa juhudi kubwa alizozifanya akiwa Mwakilishi
Mkazi wa AfDB hapa nchini ambapo miradi mikubwa na muhimu katika maendeleo
imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa.
Akizungumza baada
ya kuagana na Rais Magufuli Dkt. Tonia Kandiero amemshukuru Rais Magufuli na
Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano alioupata katika kipindi cha miaka 6
aliyokuwa hapa nchini na amesema anaondoka akiwa ameiwezesha Tanzania kupiga
hatua kubwa ya kimahusiano na AfDB ambapo miradi yenye thamani ya Dola za
Kimarekani Bilioni imetekelezwa hususani katika ujenzi wa miundombinu ya
barabara.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli ameagana na Balozi
wa Cuba hapa nchini Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo anayemaliza muda wake baada ya
kuiwakilisha nchi ya Cuba kwa miaka minne.
Rais Magufuli
amemshukuru Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo kwa uhusiano na ushirikiano mzuri
aliouendeleza kati ya Tanzania na Cuba uliojengwa na waasisi Baba wa Taifa
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mhe. Fidel Castro wa
Cuba.
Mhe. Jorge Luis
Lopez Tormo amemshukuru Rais Magufuli na Serikali kwa kuendeleza uhusiano na
ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Cuba na amesema anaondoka akiwa
anaamini kuwa uhusiano kati ya nchi hizi utaendelea kuwanufaisha wananchi
ikiwemo miradi mikubwa ya maendeleo na huduma za kijamii.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
05 Desemba,
2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo aliyefika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo pamoja na ujumbe wake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitazama kitabu cha picha ya ndege aina ya Boeing 787-8 Dream liner wakati alipokuwa akisikiliza maelezo yake kutoka kwa Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo. Ndege hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 262 na itakuwa na uwezo wa kuruka kutoka nchini Marekani hadi Tanzania bila kutua mahali popote.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza kuhusiana na ununuzi wa ndege hiyo mpya aina ya Boeing 787-8 Dream liner mara baada ya kumaliza mazungumzo na Mkurugenzi wa mauzo wa Kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Cuba anayemaliza muda wake nchini George Luis Lopez Tormo aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero aliyefika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo. Dkt. Tonia ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Ukanda wa Kusini Mwa Afrika katika Ofisi zake zilizopo Afrika ya Kusini.PICHA NA IKULU .
Sign up here with your email