Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa akitoa maagizo kwa Mhandisi Mshauri Eng. Domicus
Mapunda wa Kampuni ya Ujenzi ya Mbutu Bridge JV inayojenga barabara ya
Makutano-Nata KM 50 kwa kiwango cha lami mkoani Mara wakati alipokagua
mradi huo.
Mhandisi Mshauri Eng. Domicus Mapunda
wa Kampuni ya Ujenzi ya Mbutu Bridge JV akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu mradi wa
ujenzi wa barabara ya Makutano-Nata KM 50 inayojengwa kwa kiwango cha
lami mkoani Mara wakati alipokagua mradi huo.
Ujenzi wa barabara ya Makutano-Nata KM 50 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilaya ya Butiama, mkoani Mara ukiendelea.
Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha
Musoma Bi. Faraja akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa (kushoto), ramani ya eneo la kiwanja cha ndege
hicho, alipokagua kiwanja hicho mkoani Mara.
Muonekano wa barabara ya changarawe ya kuruka na kutua ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Musoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Kiwanja cha
Ndege cha Musoma Bi. Faraja kuhusu eneo litaloongezwa kiwanja hicho, mkoani Mara.
………….
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa amewapa miezi minne Wakandarasi Wazawa wa Kampuni
ya Ujenzi ya Mbutu Bridge JV inayojenga barabara ya Makutano-Nata
kukamilisha km 18 kati ya 50 za barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Agizo hilo limetolewa na Waziri huyo,
alipokuwa akikagua mradi huo wa barabara inayoanzia makutano kupitia
Butiama, Nyamuswa hadi Sanzate ambao upo katika mkoa wa Mara, na
kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake ambayo imesuasua kwa takriban miaka
3 sasa.
“Nataka mwezi Aprili mwakani sehemu ya
barabara hii iwe imeshakamilika kwa kiwango cha lami na wananchi waanze
kufurahia matunda yake, hatuwezi kusubiri kwa muda wote huo kuwavumilia
kukamilisha mradi huu”, amesema Prof. Mbarawa.
Amesisitiza kuwa nia ya Serikali ya
kuboresha barabara hiyo ni kupunguza gharama za usafirishaji, kuboresha
makazi, kukuza uchumi kwa maeneo yaliyo kando ya Barabara hiyo na
kuhamasisha utalii kwenye mbuga za Wanyama za Serengeti na Ngorongoro.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini
(TANROADS), Mkoa wa Mara Eng. Japherson Nnko amesema kuwa barabara hiyo
itakapomalizika itakuwa na njia ya magari yenye upana wa mita6.5, mabega
ya barabara ya mita 1.5 kila upande na Daraja kubwa la Kyarano lenye
urefu wa mita 37.5.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema
itawapa kipaumbele makandarasi wazawa kuweza kushiriki katika mradi wa
ujenzi wa reli mpya ya kisasa (Standard Gauge), inayotarajiwa kuanza
hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Serikali imewataka Makandarasi hao
kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa kwa kuomba zabuni za ujenzi huo
na kuziimarisha kampuni zao ikiwemo kuwa na vifaa vilivyo bora ili
kupambana na soko la kibiashara na makandarasi wa nje.
Sambamba na hayo, Waziri Prof. Mbarawa
amekagua Uwanja wa Ndege wa Musoma na kusema kuwa Serikali imejipanga
kuhakikisha inapanua na kujenga kwa kiwango cha lami uwanja huo hususani
njia ya kuruka na kutua ndege kutoka KM 1.6 ya sasa hadi KM 1.8 ili
kuruhusu ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba abiria 70 kutua katika
uwanja huo.
Waziri Prof. Mbarawa amemaliza ziara yake
ya siku mbili mkoani Mara ambapo amekukagua miradi mbalimbali
inayotekelezwa na Wizara yake katika Wilaya ya Bunda, Butiama, Musoma
Mjini na Serengeti.
Imetolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Sign up here with your email