Mwandishi
wa habari wa Kituo cha ITV mkoani Arusha, Khalfan Lihundi, anashikiliwa
na polisi katika Kituo cha Polisi Usa River, wilayani Arumeru kwa
tuhuma za kuandika habari zinazodaiwa kuwa ni za uchochezi.
Lihundi
alikamatwa jana jijini hapa majira ya saa nane mchana na askari
anayedaiwa kutumwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti.
Mmoja
wa waandishi wa habari walioshuhudia tukio hilo, Basil Elias, alisema
kuwa, walipokuwa ofisini, alifika ofisa wa polisi akidai ametumwa
kumfuata Lihundi kwa ajili ya mahojiano.
Kwa
mujibu wa Elias ambaye alimnukuu ofisa huyo wa polisi, Lihundi anadaiwa
kuandika habari ya uchochezi kuhusu mgogoro wa maji bila kumhoji mkuu
huyo wa wilaya.
“Habari hiyo inayodaiwa kuwa ni ya uchochezi, ilikuwa ni malalamiko ya wananchi juu ya tatizo la maji katika wilaya hiyo,” alisema Elias.
Akizungumzia
tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari, Mkoa wa
Arusha (APC), Claud Gwandu, pamoja na kulaani tukio hilo, alisema hatua
hiyo haikubaliki kwani haikufuata taratibu za kuadhibu mwandishi wa
habari.
“Hili
ni tukio la kulaani na halikubaliki kwani kama mwandishi amekosea,
zinapaswa kufuatwa taratibu na siyo kukamatwa kama mhalifu.
“Kilichofanyika
ni matumizi mabaya ya madaraka, hivyo viongozi wa kuteuliwa hasa wakuu
wa wilaya, wawe na utaratibu wa kufuata taratibu kwani mwandishi
akikosea, kuna taratibu za kufuata, tunachotaka apewe dhamana,”alisema Gwandu.
Naye Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema amesikia kuna mwandishi amekamatwa kwa kosa la uchochezi.
“Mkuu
wa wilaya ametumia mamlaka yake ya sheria inayomruhusu kumweka ndani
mtu hadi saa 48. Kwa hiyo, siwezi kuingilia kati suala hilo,” alisema Kamanda Mkumbo.
Sign up here with your email