Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi,Marcelin Ndimbwa amemwandikia mwenyekiti wa Halmalmashauri Mh. Nasoro Liguguda na baraza lake, kubadilisha matumizi kiasi cha fedha shilingi milioni 100 alizotengewa kwa ajili ya ununuzi wa gari ya mkurugenzi na kuzielekeza katika ujenzi wa Zahanati tatu.
Akizungumza na globu ya jamii ofisini kwake mapema leo asubuhi Ndimbwa amesema kuwa ameamua kufanya hivyo kutokana na mahitaji ya huduma za afya katika Wilaya hiyo kuliko yeye kununuliwa gari ya kifahari huku wananchi wakiwa wanateseka.
“nimemwandikia mwenyekiti wa Halmashauri barua juu ya kubadili matumizi ya fedha hizo kwani nimeona wazi kuwa mahitaji ya Zahanati katika wilaya yangu ni makubwa kuliko hiyo gari kwani Malinyi inahitajika kuwa na zahanati 33 lakini mpaka sasa zipo zahanati tisa tu jambo ambalo linawafanya watu kutembea umbali mrefu kufata huduma za afya”amesema Ndimbwa.
Amesema kuwa ujenzi wa Zahanati hizo unaanza mara moja katika vijiji vilivyo ainishwa na tayari wananchi walishaanza kukusanya nguvu kwa kujitolea Mchanga ,Mawe na Matofali.
Ameweka wazi kuwa pindi ujenzi huo utakapoanza hautasimama, kwani kutokana na fedha hizo na nguvu ya wananchi iliyopo kila kitu kitakamilika kwa muda muafaka na wananchi watapata huduma kama ilivyo katika matarajio yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Nasoro Liguguda amesema kuwa ameridhia uamuzi huo kutokana na sera ya serikali na ilani ya chama cha mapinduzi kuitaka kila kata kuwa na kituo cha afya na kila kijiji kuwa na zahanati moja kama mkurugenzi ameona gari sio ya muhimu na zahanati ndio ya msingi sisi tunashukuru.
Amesema kuwa wanampongeza Mkurugenzi kwa uamuzi huo kwani ni viongozi wachache wenye kariba kama yake ya kufikiria wananchi kwanza kuliko yeye, kwani angekuwa mwanasiasa ningeona kawaida lakini yeye ni mtendaji lakini bado amekuwa na uchungu na watu wa malinyi kuliko mtu mwingine yoyote hivyo sisi tunamuombea awe na moyo huohuo na aishi muda mrefu katika wilaya yetu.
Sign up here with your email