Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dr. Moses Kusiluka akisoma hotuba ya
kufungua rasmi Kongamano na Mkutano Mkuu wa Baraza la Wahitimu wa Chuo
Kikuu Ardhi lililofanyika jijini Dar es Salaam katika viwanja vya chuo
hicho.
Makamu wa Rais wa Baraza la
Wahitimu wa Chuo Kikuu Ardhi, Prof. Aldo Lupala (kushoto). Rais wa
Baraza hilo, Haruna Masebu (katikati), kulia ni Makamu Mkuu wa chuo
hicho, Prof, Idrissa Mshoro wakisikiliza kwa makini hotuba ya Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dr. Moses
Kusiluka wakati wa mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam katika
viwanja vya chuo hicho.
Baadhi ya wanachama wa Baraza la
Wahitimu wa Chuo Kikuu Ardhi wakisikiliza kwa makini wakati wa mkutano
mkuu wa baraza hilo uliofanyika jijini Dar es Salaam katika viwanja vya
chuo hicho.
……………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Ukuaji wa nchi na maendeleo yake
huchangiwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi unaotekelezwa na
wananchi hasa wale wanaohusika katika shughuli za ujenzi wa miundombinu.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Dr. Moses Kusiluka alipokuwa akifungua rasmi Kongamano na
Mkutano Mkuu wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu Ardhi lililofanyika
katika viwanja vya chuo hicho.
Dr. Kusiluka amesema kuwa ni
muhimu kwa taifa kutazama mipango ya matumizi ya ardhi kama mbinu moja
wapo itakayochochea maendeleo ya nchi, hivyo ametoa rai kwa kila
mwananchi kulitilia mkazo suala hilo ili kuhakikisha nchi inapiga hatua
za kimaendeleo.
“Kama zilivyo hatua nyingine za
maendeleo ya nchi zikiwemo za kiuchumi, kijamii na kisiasa basi mpango
bora wa matumizi ya ardhi pia ni sehemu isiyotakiwa kutengwa katika
hatua za kukuza nchi,”alisema Dr. Kusiluka.
Dr. kusiluka amekipongeza chuo
hicho kwa kushirikiana na Serikali pamoja na jamii katika kuboresha
sekta ya ardhi pamoja na sekta ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali kwa
kutoa elimu bora kwa wanafunzi ambao watakuja kuwa wataalam wazuri kwa
siku zijazo.
Kwa upande wake Rais wa Kongamano
na Mkutano Mkuu wa Baraza la Wahitimu wa Chuo hicho, Haruna Masebu
amesema kuwa lengo la kuanzshwa kwa kongamano pamoja na baraza hilo ni
kutafuta pesa kwa ajili ya kufanyia kongamano, kuandika machapisho
yanayohusiana na maudhui yanayofundisha katika chuo hicho pamoja na
kutumika kama daraja linalowaunganisha wahitimu waliomaliza miaka ya
nyuma pamoja na waliopo sasa katika chuo hicho.
“Mada inayojadiliwa katika
kongamano hili inahusu ardhi, haki za ardhi, usawa pamoja na maendeleo
yake ambapo majadiliano hayo yanalenga kuwajengea uelewa wahitimu hao
katika kukuza na kuboresha sekta nzima ya ardhi na ujenzi kwa ajili ya
kukuza maendeleo ya nchi nzima,” alisema Masebu.
Baraza hilo linalofanyika kila
mwaka limeanzishwa tangu Disemba 12 mwaka 2012 na inakadiriwa kuwa na
wanachama zaidi ya 500, ili kukuza kongamano linalosimamiwa na Baraza
hilo ni lazima kila mwanachama kuchangia shilingi 20,000 ya ada ya
uanachama pamoja na shilingi 50, 000 ya ada ya mwaka.
Sign up here with your email