Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru wanachama watano wa Chadema
pamoja na watu wengine watatu wasio raia wa Tanzania waliokuwa
wanakabiliwa na kesi ya uhalifu wa kimtandao.
Hakimu
Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage aliwaachia huru washtakiwa hao jana chini
ya Kifungu cha 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) baada ya
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kusema hana nia ya kuendeleza mashtaka
dhidi ya washtakiwa hao.
Waliachiwa huru, baada ya Wakili wa Serikali, Elia Athanas kuomba kufutwa kesi hiyo chini ya kifungu hicho na Mahakama kuridhia.
Kesi
hiyo, imefutwa ikiwa katika hatua ya kuanza kusikilizwa kwa ushahidi wa
mashahidi wa upande wa mashtaka baada ya kukamilisha upelelezi wao na
washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali.
Katika
kesi hiyo, washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza
Oktoba 27, 2015 na kusomewa mashtaka ya makosa ya uhalifu wa kimtandao,
wakidaiwa kukusanya na kusambaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika
Oktoba 25, 2015.
Washtakiwa hao ni Mashinda Edwin Mtei, Julius Mwita, Fredrick Eddie Fussi, Meshack Carlos Mlawa na Anisa Nicholaus Rulanyaga.
Mbali
na wanachama hao wa Chadema, washtakiwa wengine ambao ni raia wa kigeni
ni Julius Mwonga Matei (Kenya), Jose Mavinga Nimi ambaye kwa sasa ni
marehemu (Angola) na Kim Hyunwook (Korea) kwa pamoja wanadaiwa kutenda
makosa hayo kinyume cha Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Uhalifu
wa Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Kwa
pamoja, walidaiwa kuwa kati ya Oktoba 25 na 26, 2015 kwenye maeneo
tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walichapisha matokeo ya uchaguzi
wa urais wa mwaka 2015 yasiyo sahihi na ambayo hayakuthibitishwa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kwa lengo la kuipotosha jamii.
Walidaiwa
kuwa siku hiyo ya tukio, walichapisha na kusambaza matokeo hayo kupitia
mfumo wa uratibu wa uchaguzi uitwao ‘M4C Election Results Management’
na kupitia mitandao mingine ya kijamii, kama vile Facebook na Twitter.
Washtakiwa
Matei, Mavinga na Hyunwook wanadaiwa kujihusisha na ajira nchini bila
ya kuwa na kibali, kinyume cha Sheria ya Uhamiaji. Wanadaiwa kuwa Oktoba
26, 2015 katika Hoteli ya King D, iliyoko wilayani Kinondoni, Dar es
Salaam, wageni hao walijihusisha katika ajira ya kukusanya na kusambaza
matokeo ya uchaguzi wa urais nchini kwa Chadema bila kibali.
Pia
wageni hao walidaiwa kujihusisha na shughuli za biashara nchini kwa
niaba ya Wanama Saccos, bila ya kuwa na kibali kinyume cha Sheria ya
Uhamiaji.
Sign up here with your email