MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemwachia huru Mhandisi Mkuu wa
Mradi wa Umeme Vijijini (REA), Theophillo Bwekea, baada ya Jamhuri
kuonyesha haina nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Bwekea
alikuwa akituhumiwa kupokea rushwa ya Sh milioni 161.7 kutoka kwa
Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira.
Wakili
wa Serikali, Odossa Olombe, alidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Respiciou Mwijage kwamba upelelezi wa kesi hiyo
haujakamilika.
Hivyo
aliomba kuondoa kesi hiyo chini ya kifungu cha sheria namba 98(a) cha
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) aya ya 20 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Hakimu
Mwijage aliyakubali maombi ya upande wa Jamhuri na kuamuru mshtakiwa
kuachiwa huru chini ya kifungu cha sheria namba 98(a) cha CPA.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka Januari 20, 2015.
Wakili
wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai, awali akisoma mashtaka
alidai kuwa mshtakiwa anatuhumiwa kupokea rushwa ya Sh 161,700,000
kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira,
ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwamo kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kabla
ya kufanya kazi REA, Theophillo alikuwa Wizara ya Nishati na Madini,
kitengo cha kusimamia umeme, ambako anadaiwa alishiriki kutunga sera ya
kampuni binafsi kuuza umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na
ilipoanza kutumika, Kampuni ya kufua umeme ya IPTL ilikuwa ya kwanza
kupata zabuni.
Wakili
Swai, alidai Februari 12, 2014 katika Benki ya Mkombozi, mshtakiwa
akiwa Mhandisi Mkuu wa REA, kwa rushwa alijipatia Sh milioni 161.7
kupitia akaunti namba 00410102643901 fedha ambazo ni sehemu ya
zilizokuwapo katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Alidai
fedha hizo aliingiziwa katika akaunti yake na Rugemalira ambaye ni
mshauri binafsi wa kimataifa, Mkurugenzi wa VIP Engineering na alikuwa
Mkurugenzi wa IPTL.
Fedha
hizo zinadaiwa alipewa zawadi kwa kuwa alikuwa mmoja wa wajumbe
walioandaa sera zilizoruhusu sekta binafsi kuuza umeme Tanesco.
Mshtakiwa
huyo alikuwa nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na
wadhamini wawili ambao ni watumishi wa Serikali ama kutoka taasisi
inayotambulika waliotakiwa kuwa na barua za utambulisho na kila mmoja
kusaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 25.
Sign up here with your email