LUKUVI ATOA HATI 154 KWA WAKAZI WA BUNDA MKOANI MARA - Rhevan Media

LUKUVI ATOA HATI 154 KWA WAKAZI WA BUNDA MKOANI MARA


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimkabidhi Hati 154 za Kumiliki Ardhi kwa wakazi wa wilaya ya Bunda Mkoani Mara wakati alipofanya ziara ya siku mbili ya utatuzi wa Migogoro ya Ardhi mkoani humo. 

Lukuvi alitoa hati hizo kwa wananchi wa Wilaya ya Bunda ili kuwarahisishia wakazi hao utaratibu wa kupata hati zao pale walipo badala ya kuzifuata Mkoani Mwanza katika ofisi za Kamishana Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwawa.

Aidha, Katika ziara hiyo Waziri Lukuvi ametatua migogoro ya Ardhi ya wananchi wa Musoma mjini na wananchi wa Bunda walio na kero za migogoro ya ardhi na kuzipatia ufumbuzi pamoja na kupokea vielelezo vya kero za wananchi zaidi 300 walizoziwasilisha kwa Waziri ili azitolee maamuzi.

Waziri Lukuvi alikagua nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Buhare wilayani Musoma lenye jumla ya nyumba 50 zinazokaribia kukamilika, ambapo alimtaka Meneja wa Mradi wa NHC mkoa wa Mara Frank Mambo kukamilisha mradi huo ndani ya miezi mitatu.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi anaendelea na Ziara zake za utatuzi wa Migogoro ya Ardhi nchini, ambayo imejikita zaidi katika kutatua migogoro ya ardhi ya Mikoa ya kanda ya Magharibi, Kaskazini na ile ya Kanda ya Ziwa hapa nchini.

Aidha, Mhe. Lukuvi baada ya ziara hiyo anatarajiwa kuwasili mkoani Arusha ambapo pia atatua migogoro ya ardhi inayoukabili mkoa huo katika wilaya za Arumeru na Karatu.

Hadi sasa Mhe. Lukuvi ndani ya mwezi huu wa Desesmba ameishatatua migogoro ya ardhi ya Mkoa wa Kigoma na wilaya zake za Kigoma mjini, Kasulu na Kibondo na katika Mkoa wa Shinyanga na wilaya zake za Kishapu na Shinyanga mjini na katika mkoa wa Geita amefanya ziara katika wilayani Chato.
Na. Hassan Mabuye (Kitengo cha Mawasiliano - Wizara ya Ardhi)
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimkabidhi Hati ya Kumiliki Ardhi Bibi Ester Lukondo mkazi wa Bunda Mkoani Mara, ambaye ni miongoni mwa wakazi 154 waliopelekewa Hati hizo na Waziri wa Ardhi Wilayani Bunda badala ya wakazi hao kuzifuata Mkoani Mwanza.
     Wananchi wa Musoma mjini wakikwasilisha Kero zao za migogoro ya ardhi kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ili aweze kuzipatia ufumbuzi.
   Wananchi wa Bunda wakikwasilisha Kero zao za migogoro ya ardhi kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ili aweze kuzipatia ufumbuzi.
  Waziri Lukuvi akikagua nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Buhare wilayani Musoma lenye jumla ya nyumba 50 zinazokaribia kukamilika.
 Jengo la Biashara la Musoma Mjini lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo Waziri Lukuvi alifika kuangalia maendeleo yake.

Previous
Next Post »