Wakati
polisi wakisema kuwa wanaufanyia mchakato wa vipimo vya vinasaba (DNA),
mwili wa mtu anayedaiwa kuuawa nje kidogo ya mji wa Moshi na kuwekwa
kwenye kiroba na kuchomwa moto, familia ya Ben Saanane, msaidizi wa
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye hajulikani aliko imesema
inaenda kuuangalia mwili huo.
Hatua
hiyo ya polisi kupima DNA ilielezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa
Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa baada ya hadi jana, mwili huo
kutotambuliwa.
Mauaji
hayo yaligunduliwa Ijumaa iliyopita, baada ya watu waliokuwa na gari
ndogo ambao hawajafahamika, kumchoma moto mtu huyo katika Kijiji cha
Ongoma na kisha kutoweka kusikojulikana.
Kamanda
Mutafungwa aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mtu huyo
hajafahamika na wala hakuna mtu aliyejitokeza kuutambua mwili huo hivyo
kulilazimu jeshi kufanya uchunguzi huo wa kisayansi.
Kamanda
Mutafungwa alitoa wito kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopotelewa na
ndugu, wafike katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kuutambua mwili huo.
Kuhusu
madai ya marehemu kwamba alikuwa amevaa suruali inayofanana na sare za
wafungwa, Kamanda Mutafungwa alisema si kweli kwani nguo iliyoonekana ni
blanketi jepesi la rangi ya chungwa.
Mzazi wa Saanane
Wakati
polisi ikijiandaa kwa mchakato huo, baba wa Saanane, Focus Saanane,
jana alikuwa anajiandaa kwenda KCMC kuangalia mwili huo.
Akizungumza
jana mjini Moshi, Saanane alisema japokuwa mtoto wake alipotelea Dar es
Salaam, watakwenda kuuangalia mwili huo ili kujiridhisha.
Juzi
Saanane alikaririwa akiiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kupotea kwa
mwanaye akisema ndiyo pekee yenye vyombo vya kiuchunguzi.
Kuokotwa
kwa mwili huo kunashabihiana na tukio la kupatikana kwa miili mingine
saba katika Mto Ruvu mkoani Pwani ikiwa imefungwa katika viroba na
kuwekewa mawe ili izame.
Miili
hiyo ilizikwa na wananchi wanaoishi jirani na mto huo bila kufanyika
kwa vipimo vya DNA wala kutoa tangazo la watu waliopotolewa na ndugu zao
kujitokeza kutambua maiti hizo hali iliyoibua utata.
Tayari
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alishaagiza kufanyika kwa uchunguzi wa
miili hiyo na kutaka wale wote waliohusika na mauaji hayo watafutwe na
kukamatwa.
Sign up here with your email