Mahakama
ya Hakimu Mkazi Tanga, imemtia hatiani na kumuhukumu kwenda jela miaka
25 au kulipa faini ya Sh bilioni 3.7 mfanyabiashara Charles Kijangwa kwa
kujihusisha na biashara ya meno ya tembo.
Kijangwa
alihukumiwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cresencia Kisongo,
baada ya kuruka dhamana kwa miaka sita. Alishindwa kulipa faini.
Mshtakiwa
huyo alikabidhiwa mahakamani hapo baada ya kukamatwa na askari wa
kikosi cha kuzuia ujangili Kanda ya Mashariki na Pwani kwa kushirikiana
na Jeshi la Polisi Wilaya ya Lushoto.
Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Saraji Iboru, alidai mahakamani kuwa mshtakiwa
Kijangwa alikuwa akitafutwa na Serikali kwa muda mrefu tangu mwaka 2010
baada ya kuruka dhamana katika shauri la uhujumu uchumi namba 6/2007.
Mshtakiwa
alishtakiwa na wenzake Michael Msuya na Nyaisa Makori ambao walitiwa
hatiani na mahakama, wakahukumiwa kwenda jela miaka mitano kwa kosa la
kumiliki kilo 5,000 za meno ya tembo kwa shtaka la kwanza.
Katika
shtaka la pili la kula njama, washtakiwa wote walihukumiwa kwenda jela
miaka mitano au kulipa faini ya Sh 10,950,000 baada ya kupatikana na
hatia ya kusafirisha kilo 5,000 za meno ya tembo kwenda nchini Taiwan
mwaka 2006.
Iboru
aliiambia mahakama kuwa washtakiwa watatu, Kijangwa na wenzake
walihukumiwa kwenda jela miaka mitano au faini ya Sh 50,000 katika
shtaka la kujihusisha na biashara ya nyara za Serikali kinyume cha
sheria.
Alidai mshtakiwa hakufika mwenyewe mahakamani hapo bali aliletwa baada ya kukamatwa Desemba 11, mwaka huu wilayani Lushoto.
Aliiomba mahakama kumtia hatiani mshtakiwa na kuhakiksha anatumikia adhabu iliyotolewa dhidi yake akiwa hayupo.
Hakimu
Kisongo baada ya kusikiliza maombi hayo, alimtia hatiani mshtakiwa na
kumuhukumu kwenda jela miaka 25 au kulipa faini ya Sh bilioni 3.7.
Mshtakiwa
Kijangwa alitenda kosa hilo Novemba 2005 na Aprili 2006 kwa kusafirisha
makontena mawili ya meno ya tembo yenye ujazo wa tani 5,000
yaliyokamatwa katika bandari ndogo ya Konshugi nchini Taiwan.
Makontena
hayo ambayo yalitokea katika Bandari ya Tanga yakiwa na shehena ya
kamba za katani na meno ya tembo ndani yake, yalikuwa yanapelekwa Manila
nchini Philipine.
Sign up here with your email