WAKENYA WAMTAMANI RAIS MAGUFULI KWA MWAKA MMOJA - Rhevan Media

WAKENYA WAMTAMANI RAIS MAGUFULI KWA MWAKA MMOJA

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Kenya (COTU), Bw. Francis Atwoli amesema anaikubalia kasi ya Rais Magufuli katika kupambana na rushwa.
Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli
Pia amewataka Watanzania wamuunge mkono badala ya kulalamikia kasi kwani wao wanatamani mwakani aende kugombea kwao katika uchaguzi mkuu ujao.
Ametoa kauli hiyo katika Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) katika ukumbi wa Mwalimu Julius K. Nyerere ulioko Chuo cha Mipango, nje kidogo ya mji wa Dodoma, uliofunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
“Ninawasihi wanaTUCTA suala la rushwa msilipe nafasi. Mpambane nayo kwa sababu kule kwetu imeota mizizi. Muungeni mkono Rais Magufuli, badala ya kulalamika kuwa kasi yake ni kubwa mno. Mnasema eti ana spidi sana, mkiona taabu mtuazime japo kwa mwaka mmoja ili aje atunyooshee mambo kule kwetu,” alisema huku akishangiliwa.

Bw. Francis Atwoli - Katibu Mkuu COTU
Amewataka wahimize uhusiano uliopo baina ya vyama vya wafanyakazi, waajiri na Serikali iliyopo madarakani na kuwataka wadumishe umoja miongoni mwa viongozi na wanachama mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
Previous
Next Post »