SIMBA YAMCHAPA BARUA RAIS WA TFF , JAMAL MALINZI - Rhevan Media

SIMBA YAMCHAPA BARUA RAIS WA TFF , JAMAL MALINZI

Uongozi wa klabu ya Simba umelitaka Shirikisho la Soka nchini TFF kukaa na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ili kuweza kujua tatizo linalochangia kutokusikilizwa kwa malalamiko yao.
Uongozi wa klabu ya Simba

Akizungumza jijini Dar es salaam, Afisa Habari wa Klabu ya Simba Haji Manara amesema, wameshapeleka malalamiko mengi kwa TFF ambapo mpaka sasa bado hayajasikilizwa hivyo wameamua kuandika barua ya moja kwa moja kwenda kwa Rais wa Shirikisho hilo Jamal Malinzi ili kujua ni nini tatizo.
Manara amesema, mpaka sasa wameshapeleka malalamiko mengi yakiwamo ya kesi ya mchezaji Hassan Kessy kusajiliwa na Yanga ilihali bado ana mkataba na Simba pamoja na ile ya Ramadhan Singano kuhusu mkataba ambao kulikuwa na mgogoro wa kujua upi mkataba feki alionao Singano au Simba.

Hassan Kessy 
Manara amesema, malalamiko mengine waliyoyapeleka TFF ni kuhusu mchezaji wao Mbaraka Yussuph ambaye walimpeleka Kagera Sugar kwa mkopo ambapo mkopo huo uliisha Juni mwaka huu na TFF imempa leseni ya kuendelea kuitumikia Kagera Sugar huku akiwa bado ana mkataba na klabu ya Simba.
Manara amesema, wanashangaa kuona mpaka sasa kesi ya mwamuzi Martin Saanya na Samuel Mpenzu waliochezesha mechi yao dhidi ya Yanga bado inafanyiwa uchunguzi ikiwa ni siku ya 52 tangu tukio litokee huku baadhi ya kesi zikitolewa maamuzi.

Jamal Malinzi - Rais TFF
Manara amesema, kutokana na matukio yaliyotokea katika mchezo huo dhidi ya Yanga, hawatakubali kucheza mechi yoyote ile dhidi ya Yanga iwapo mwamuzi wa mchezo huo atatoka hapa nchini, na wapo radhi kugharamia nauli, malazi pamoja na usafiri wa ndani kwa muamuzi ambaye atatoka nje ya nchi kwa ajili ya kuja kuchezesha mchezo wao.
Manara amesema, kumekuwa na ubadilishwaji wa ratiba ya ligi kuu bila kuwa na taarifa sahihi, hivyo watahakikisha wanapambana ili kuhakikisha hawaharibiwi ratiba ili mzunguko wa pili ligi ichezwe kwa usalama na amani.

Previous
Next Post »