VIDEO : NAWAPA MIEZI MIWILI ZIJENGWE BEACONS MBUGANI - MAJALIWA - Rhevan Media

VIDEO : NAWAPA MIEZI MIWILI ZIJENGWE BEACONS MBUGANI - MAJALIWA


Tokeo la picha la waziri mkuu

*Ni kwa ajili ya kuzuia migogoro ya mipaka na wanavijiji
*Aagiza TAMISEMI isimamishe usajili wa vijiji kuanzia leo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi na siku tisa kwa Wakuu wa Mapori ya Hifadhi za Misitu kuhakikisha wanaweka mawe ya alama (beacons) kwenye mipaka yao ili kuepusha migogoro na wanavijiji wanaowazunguka.
Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumatatu, Novemba 21, 2016) wakati akizungumza na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakuu wa Mapori ya Hifadhi za Misitu nchini katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.
“Tatizo la migogoro baina ya wafugaji, wakulima na kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya ni lazima lifanyiwe kazi. Mkitoka hapa rudini katika maeneo yenu mkawaambie wananchi mipaka yenu iko wapi. Ninyi mnatambua mipaka yenu iko wapi kwa hiyo waelewesheni wananchi kwa kuweka alama,” amesema.
“Wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli akizindua bunge tarehe 20 Novemba, 2015 aliwapa maeneo makuu matatu ambayo ni kuanisha mipaka, kupambana na ujangili na kukusanya mapato. Alizungumzia suala la mipaka kwa sababu iliyopo haieleweki, mkiulizwa mnajibu kuna buffer zone. Hivi mwananchi wa kawaida anajua buffer zone ni nini?,” alihoji.
“Sasa ninawapa muda hadi Januari 31, 2017 kazi ya kuweka beacons kwenye hifadhi zote za misitu iwe imekamilika. Kila pori nenda mkatengeneze alama zenu kama TANROADS walivyofanya. Kaeni mpige hesabu ni kiasi gani cha saruji na kokoto kinahitajika. Tutarudi hapa Dodoma kupeana taarifa ya utekelezaji. Katibu Mkuu niletee taarifa ya kila mkoa na wilaya kuna mapori mangapi tutakutana hapahapa kupeana mrejesho,” alisisitiza.
Alisema kama TANROADS waliweza kuweka alama za barabarani kwa nchi nzima ni kwa nini Wizara ya Maliasili na Utalii imeshindwa kuchukua hatua kama hizo. “Ni lazima tuweke hizo alama kila katika pori lake, tusipofanya hivyo, migogoro hii itaendelea,” alisema.

Previous
Next Post »