Serikali imesema itahakikisha inaimarisha uwezo wa kitaasisi ili kumudu vyema kazi za ufuatiliaji na tathmini ikiwa ni pamoja na kutoa miongozo mbalimbali itakayosaidia kuboresha utendaji kazi za Ufuatiliaji na tathmini serikalini.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Susan Mlawi alipokuwa akifungua Mafunzo ya siku mbili ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa Wizara mbalimbali yanayofanyika Ofisi ya Rais-Utumishi.
Mlawi alisema Mkakati wa Serikali wa kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini kwa taasisi hizo kunatonakana na kukosekana kwa mfumo madhubuti wa Ufuatiliaji na Tathmini ambao ungetoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazozikabili Taasisi za Umma nchini.
“Kukosekana kwa mfumo madhubuti wa Ufuatiliaji na Tathmini katika taasisi za umma nchini umesababisha kukwama kwa utekelezaji wa majukumu ya kila siku na utoaji maamuzi sahihi,”
Bi. Mlawi aliongeza. Alidha, Kaimu Katibu Mkuu huyo alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili Serikali kuwa ni pamoja na baadhi ya taasisi zake kulalamikiwa na wananchi kwa kutoa huduma zisizoridhisha, utendaji ambao haulingani na thamani halisi ya uwekezaji wa fedha za Umma katika taasisi hizo, mchango mdogo wa baadhi ya Taasisi za Umma katika kuchangia mapato katika Mfuko Mkuu wa Serikali, ongezeko la utegemezi kwa Serikali kuu, uzalishaji na tija ndogo na ukosefu wa vipaumbele katika taasisi hizo.
Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Ushauri wa Kazi wa Ofisi ya Rais-Utumishi, Bw. Mick Kiliba akitoa maelezo kuhusu Mafunzo ya siku mbili ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa Wizara mbalimbali yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Rais-Utumishi.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi Susan Mlawi, akifungua Mafunzo ya siku mbili ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa Wizara mbalimbali yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Rais-Utumishi.
Baadhi ya washiriki kutoka Wizara Mbalimbali wakifuatilia mada wakati wa Mafunzo ya Ufuatiliaji na Tathmini yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Rais-Utumishi.
Sign up here with your email