KISUTU YAMUONYA LISSU, YASEMA HAIMWOGOPI - Rhevan Media

KISUTU YAMUONYA LISSU, YASEMA HAIMWOGOPI

Tokeo la picha la TUNDU LISSU MAHAKAMANI

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema haimuogopi kumwadhibu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na  imemuonya tabia yake ya kushindwa kufuata taratibu za kisheria anapokuwa na udhuru siku kesi yake inapopangwa kusikilizwa.

Kadhalika imesema Lissu anatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii, mshtakiwa huyo alishindwa kufika mahakamani mara tatu mfululizo kusikilizwa kesi yake na wenzake watatu dhidi ya mashtaka ya uchochezi kupitia gazeti la Mawio.

Onyo hilo lilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya mahakama yake kutoa amri ya kukamatwa Lissu Novemba 3, mwaka huu.

"Pamoja na nafasi yako uliyonayo kwa jamii lakini ujue kwamba mahakama hatukuogopi labda upande wa Jamhuri ulioshindwa kuja kukukamata ... mahakamani hakuna kuoneana bali taratibu za kisheria zinachukua mkondo wake" alisema Hakimu Simba.

ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya hakimu na Lissu:
Hakimu Simba ; Awali ulikwenda Ujerumani bila kutoa taarifa mahakamani unadhani tunakuogopa?

Lissu; Sina nia mbaya mheshimiwa hakimu nilipelekwa Ujerumani kwa dharula.

Hakimu Simba ; Je, kesi ya Uchaguzi wa Jimbo la Bunda nayo ilikuwa ni dharula?

Lissu; Mheshimiwa hakimu nilipotoka Ujerumani nilikuta kesi ya Bunda imepangwa kusikilizwa na ilikuwa na muda maalumu, niliandika barua Hakimu Mfawidhi wa mahakama hii ya Kisutu na nakala nilielekeza kwa upande wa Jamhuri sina nia ya kuidharau mahakama.
Hakimu; Kutokana na nafasi yako katika jamii ujue kwamba mahakama hatukuogopi labda upande wa Jamhuri ulioshindwa kukukamata na kukuweka chini ya ulinzi.



Previous
Next Post »