Jeshi
la Polisi linafanya uchunguzi namna mtu mmoja alivyofuatiliwa na watu
wasiojulikana alipotoka benki kuchukua fedha hadi wakampora mfuko
uliokuwa na kiasi cha Sh15 milioni muda mfupi baada ya kufika nyumbani
kwake.
Naibu
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Ernest Matiku alisema wana
taarifa za tukio la wizi huo uliofanyika Ijumaa iliyopita baada ya mteja
huyo kutoka Benki ya NMB Tabata na wanalifanyia kazi kubaini wahalifu
hao.
Tukio
hilo ni moja ya matukio ambayo katika siku za karibuni watu mbalimbali
wamekuwa wakiporwa fedha na watu wenye silaha, ikiwa ni muda mfupi baada
ya kutoka benki, hali ambayo inajenga wasiwasi juu ya sehemu ambazo
majambazi hao hupata taarifa za watu wanaokwenda benki kuchukua fedha.
Hofu
miongoni mwa wateja imezidi kutokana na tukio lililotokea Ijumaa ya
wiki iliyopita ambapo majambazi wakiwa na pikipiki mbili walimfuatilia
mteja aliyetoka kuchukua fedha benki kiasi cha Sh15 milioni na kumpora
mbele ya nyumba yake.
Akisimulia
tukio hilo mwathiri- ka wa wizi huo, alisema alichukua fedha kwenye
tawi la NMB Tabata kisha akapanda daladala akaenda kushuka kituo cha
Tabata Bima.
Alisema
alipokuwa anaelekea nyumbani kwake hakuwa na shaka, lakini alipokaribia
alihisi kuna mtu anamfuata ingawa hakumuona, hivyo aliingia kwenye baa
iliyokuwa njiani na kutokea upande wa pili kwa kutumia uchochoro
uliokuwapo.
Alisema baada ya kutokea upande wa pili aliangaza kushoto na kulia hakuona mtu kisha aliamua kuongoza hadi nyumbani kwake.
“Nilipofika
hapo nje kwenye mwembe (umbali wa mita tatu kuingia ndani ya nyumba
yake), nikakuta watu wanne wakiwa na pikipiki mbili wamesimama mbele
yangu,” alisimulia akiwa nyumbani kwake muda mfupi baada ya kuruhusiwa Hospitali ya Muhimbili alikokuwa anapatiwa matibabu.
“Wakanitaka
niwape fedha ambazo zilikuwa kwenye mfuko nimezishika mkononi. Kabla
sijakaa vizuri wakapiga risasi hewani, kutahamaki wakanipiga juu ya goti
la mguu wa kulia ikaniparaza, lakini nilikuwa bado nimeng’ang’ania ule
mfuko wenye fedha,” alisema.
Aliendelea
kueleza kuwa baada ya kuona hana mpango wa kutoa fedha, wakampiga
risasi mguu huo huo chini ya goti ikapasua mfupa mkubwa na kutokea
upande wa pili na kumnyang’anya mfuko wa fedha.
“Hakuna mtu aliyekuwa anafahamu suala hilo zaidi ya mimi mwenyewe,” alisema huku akiugulia maumivu.
Sign up here with your email