Asifiwe George na Paulina Kebaki (TUDARCO), Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewakamata majambazi sugu wanne wakiwa na silaha tatu za kivita katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Hezron Gyimbi, jana aliwaambia waandishi kuwa silaha zilizokamatwa ni bastola tatu, moja aina ya Chinese na Browning mbili zikiwa na risasi 21.
Kamanda Gyimbi alisema majambazi waliotiwa mbarani walinaswa katika maeneo tofauti ya jijini na alimtaja wa kwanza kuwa ni Hamis Mjeta (40) aliyekamatiwa Temeke.
Aliwataja wengine kuwa ni Abasi Amiri (25) mkazi wa Kinondoni Mosgue aliyekutwa na bastola aina ya Browning yenye namba A.981652 na risasi 15 ndani ya magazine iliyotengenezwa nchini Czechoslovakia.
Kamanda Gyimbi alimtaja pia Gimanwa Petro (30) ambaye alikamatwa eneo la Mbagala, Mto Mzinga akimiliki silaha kinyume cha sheria na kubaini kuwa anaitumia kufanya matukio ya ujambazi.
“Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa ili kubaini silaha hizo walizipata wapi na upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa kwa mwanasheria mkuu wa Serikali kwa ajili ya hatua za kisheria,” alisema Kamanda Gyimbi.
Sign up here with your email