SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema sakata la
mkataba tata kati ya kampuni ya Lugumi Interprises Limited na Jeshi la
Polisi bado halijaisha na litajadiliwa bungeni katika mkutano ujao
utakaoanza Septemba 6.
Kampuni hiyo ilikuwa inatekeleza mradi wenye thamani ya Sh. bilioni
37 wa kusimika mfumo wa utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya
polisi nchi nzima, baada ya kushinda zabuni hiyo miaka sita iliyopita.
Katika mahojiano na moja ya vituo vya televisheni vya jijini Dar es
Salaam jana, Ndugai alisema suala hilo bado halijamalizika kwa kuwa
kamati ndogo iliyoundwa kulifanyia uchunguzi inatakiwa kutoa taarifa
bungeni.
“Na imeelekezwa sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali(CAG) kupita kuhakikisha vifaa vipo na vinafanya kazi na taarifa
itakuja kwenye mkutano ujao wa bunge ambao wapinzani watakuwapo na
wabunge wa CCM watakuwapo,”alisema Ndugai.
Alisema moja ya shughuli zitakazofanyika katika mkutano huo ni
taarifa za kamati ndogo iliyoundwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC) kuchunguza suala hilo.
Aprili 23, mwaka huu, PAC iliunda kamati ndogo hiyo ya watu tisa
kuchunguza utekelezaji wa mradi huo na taarifa yake inatakiwa
kuwasilishwa bungeni.
Kulikuwa na mkanganyiko, hata hivyo, baada ya Naibu Spika, Dk. Tulia
Ackson kuagiza serikali ikamilishe utekelezaji wa mradi ndani ya miezi
mitatu kuanzia Juni 30.
Sign up here with your email