SERIKALI YA ZNZ YATAJA KILICHOMUUA RAIS WA PILI WA SMZ ABOUD JUMBE,KESHO KUZIKWA !! - Rhevan Media

SERIKALI YA ZNZ YATAJA KILICHOMUUA RAIS WA PILI WA SMZ ABOUD JUMBE,KESHO KUZIKWA !!


Rais wa Awamu ya Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Aboud Jumbe amefariki dunia leo mchana nyumbani kwake Kigamboni jijini Dar es salaam.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Mohamed Abood amethibitisha kifo hicho, na kuongeza kuwa maziko yatafanyika kesho visiwani Zanziabr baada ya mwili wake kusafirishwa kutoka Dar es salaam, leo hii.

Amesema bado haijafahamika kilichosababisha kifo hicho, isipokuwa anafikiri kinaweza kuwa kimesababishwa na maradhi yatokanayo na umri.

"Ni ngumu kusema sababu za kifo lakini pengine ni uzee, maana umri wake ulikuwa umekwenda"
Amesema taarifa rasmi ya serikali itatolewa baadaye na kuwataka wazanzibari wakiwemo ndugu jamaa na viongozi mbalimbai kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi

Aboud Jumbe Mwinyi alizaliwa Tarehe 14 mwezi Juni mwaka 1920, na amefariki leo tarehe 14 Agosti mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 96.

Wakati wa uhai wake alishika nyazifa mbalimbali ikiwemo ya urais wa awamu ya pili wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Zanzibar.

Alikuwa Rais wa Zanzibar kuanzia April 11 mwaka 1972 hadi tarehe 30 Januari mwaka 1984 akichukua nafasi ya Rais wa Kwanza wa nchi hiyo Abeid Karume aliyeuawa April 7, 1972.

Alishika nafasi hiyo ya urais kwa kuhaguliwa na Baraza la Mapinduzi wakati huo likiwa chini ya chama cha ASP kabla hakijaungana na TANU na kuzaa Chama Cha Mapinduzi mwaka 1977.


Mwaka 1979, Jumbe alisukuma mabadiliko ya Katiba yaliyotenganisha majukumu kati ya Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi.

Mabadiliko mengine yaliyofanyika katika katiba ni kuwezesha wananchi kumchagua Rais kupitia uchaguzi wa kidemokrasia badala ya utaratibu uliokuwepo ambapo Rais alikuwa akichaguliwa na Baraza la Mapinduzi.

Jumbe atakumbukwa kwa kuwa kiongozi mwenye msimamo thabiti katika kusimamia maamuzi yake na serikali, wakati wa uhai wake.
Previous
Next Post »