NATAFUTA DAWA YA MAZEMBE - PLUIJM - Rhevan Media

NATAFUTA DAWA YA MAZEMBE - PLUIJM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm amesema amefurahishwa na ushindi wa kwanza ilioupata timu yake dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria na sasa anaangalia namna ya kuifunga TP Mazembe ya Congo DR.
Yanga juzi ilipata ushindi wake wa kwanza kwenye hatua ya makundi ya michuano ya kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilifunga bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi nne lakini ikisubiri matokeo mabaya katika mechi ya Mo Bejaia na Medeama ya Ghana huku yenyewe ikiomba iishinde Mazembe mjini Lubumbashi.
Akizungumza baada ya mechi hiyo juzi, Pluijm alisema amefurahishwa na ushindi huo na kwamba kikosi chake kilistahili kuupata kwa vile kilicheza vizuri hasa katika dakika 15 za mwanzo.
“Dakika 15 za mwanzo walicheza vizuri na kupata bao la mapema lakini baadae walicheza kwa presha kubwa… kipindi cha pili walicheza vizuri ila walikuwa na matatizo hasa kwenye safu ya ushambuliaji kwa kushindwa kupata magoli mengi, licha ya kutengeneza nafasi nyingi,” alisema.
Aliimwagia sifa Bejaia kwa kucheza vizuri na kusema ina wachezaji wazuri wa kimataifa na kwamba safu ya ulinzi ya Yanga ilifanya kazi ya ziada kuzuia washambuliaji wa timu hiyo.
“Sasa naangalia mbele kuona jinsi nitakavyopata ushindi kwa Mazembe kwenye mechi yetu ya mwisho,” alisema Pluijm.
Previous
Next Post »