JIM Nyamu, Raia wa Kenya anayezunguka nchi tatu katika Afrika Mashariki (Kenya, Tanzania na Uganda), akitoa elimu kuhusu uwindaji haramu wa tembo na kifaru, ameipongeza Tanzania kwa kuunga mkono juhudi za kupambana na majangili wanaoteketeza tembo na kizazi chake, anaandikaMoses Mseti.
Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni mara baada ya kumaliza matembezi ya kilomita 13 yaliyozinduliwa na John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza yalioanzia Kamanga Feri hadi Kona ya Nyegezi, jijini Mwanza.Nyamu amesema, anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuweka sheria kali kwa watu wanaopatikana na makosa ya ujangili kitendo ambacho amedai kimesaidia kupunguza tatizo hilo.
“Naishukuru serikali yenu kwa kuunga mkono matembezi haya, lakini inaonesha jinsi gani ambavyo inapinga ujangili unaosababisha tembo wengi kuuawa pamoja na kifaru.
“…nimeanza matembezi haya Juni 4, mwaka huu nchini Kenya, leo (juzi) ni siku yangu ya 90 kuwa hapa Mwanza, tushirikiane kuwalinda tembo,” amesema Nyamu.
Amesema, kuenea kwa ujangili katika nchi tatu za Afrika Mashariki, kunatokana na nchi ya Zimbabwe, Namibia na Botswana kuruhusu kwa kutoa vibali vya uwindaji tembo, hivyo kuwapa mwanya majangili kujiingiza katika hizi tatu na kuua tembo na faru.
Junaid Kaderi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Exotic Expeditions ya jijini Mwanza ambayo ilimdhamini Nyamu katika matembezi hayo amesema, kitendo anachofanya Mkenya huyo kutasaidia kuongeza watalii nchini, hivyo kuipatia zaidi mapato sekta hiyo.
“Tumeamua kumdhamini Nyamu kwa lengo la kuhamasisha kupinga uwindaji haramu wa tembo na faru, kwani elimu inayotolewa kwa jamii itasaidia kuwalinda wanyamapori hao,” amesema Kadri.
Hata hivyo, Kadri ameshukuru mashirika mengine kusaidia kuwaunga mkono kumsapoti Mkenya huyo, ikiwamo bodi ya utalii, hifadhi ya wanyamapori na mkuu wa mkoa wa Mwanza, lakini alisikitika shirika la hifadhi la taifa (Tanapa), kutoshiriki licha ya kupewa taarifa.
David Kabambo, Mkurugenzi la Shirika la Peace for Conservations la jijini Mwanza amesema, jamii inatakiwa kushirikiana kuwalinda wanyamapori kutokana na wale wa vijijini kushirikiana na wa mjini katika kuwaangamiza tembo.
“Jamii ya vijijini ndiyo kwa asilimia kubwa inahusika na mauaji ya tembo, lakini mipango yote inafanywa na watu wa mijini ambao wanafadhili kwa kutoa pesa, hivyo lazima tushirikiande kwa pamoja kuwalinda wanyama hawa,” amesema Kabambo.
Hata hivyo, Mongella amesema tembo na kifaru wana thamani kubwa, hivyo lazima kila jamii iweze kuwalinda ili kulinda utalii nchini, kwani asilimia kubwa ya mapato ya nchi yanatokana na sekta hiyo.
“Namshukuru sana Nyamu kwa matembezi haya aliyoyandaa katika nchi tatu, naamini jamii itaelimika na kuwalinda wanyama hawa…tutoe taarifa pale unaposikia ama kuona kuna watu wana mpango wa kuwaua,” alisema Mongella.
Sign up here with your email