LEMA AAHIRISHA MKUTANO - Rhevan Media

LEMA AAHIRISHA MKUTANO

MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) amesema hawezi kufanya mkutano wake wa hadhara Agosti 20, mwaka huu, kwa vile kibali chake kwa Jeshi la Polisi mkoani Arusha kina masharti magumu.
Lema alisema hayo jana mbele ya waandishi wa habari na kuamua kuahirisha mkutano wake wa hadhara jimboni Arusha uliokuwa ufanyike katika viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro.
Alisisitiza kuwa hawezi kufanya mkutano bila kuwashirikisha wadau wa chama chake, wakiwemo wabunge marafiki kwani hatua hiyo inakaribisha ukabila na ukanda kwa kutaka kila mbunge afanye mikutano katika jimbo lake.
Lema alisema kibali alichokabidhiwa na Jeshi la Polisi kilimruhusu afanye mkutano katika eneo hilo kwa sharti la kutomshirikisha mtu yeyote kutoka nje ya jimbo lake kuhutubia katika mkutano huo, jambo alilodai ni unyanyasaji na ukandamizaji wa uhuru wa kidemokrasia.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo alieleza kukerwa na matumizi mabaya ya ving’ora katika barabara za Arusha akidai misafara yenye ving’ora imevamiwa na watu wasiostahili kisheria.
Alitaka serikali itoe ufafanuzi kuwa nani mwenye mamlaka ya kutumia msafara wenye ving’ora kisheria kwa kuwa hivi sasa mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa, waziri na naibu waziri, wamekuwa wakitumia ving’ora katika misafara yao na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara jijini Arusha.
Previous
Next Post »