ENEO LA IKULU LAUZWA. - Rhevan Media

ENEO LA IKULU LAUZWA.



ENEO lililokuwa limetengwa ili ijengwe Ikulu ndogo ya Mkoa wa Mbeya limemegwa na kuuzwa. Limeuzwa kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni maofisa wa ardhi Jiji la Mbeya, kutumia fursa ya eneo hilo kujinufaisha kwa kuuza viwanja.

Inaelezwa kuwa baadhi ya maofisa ardhi wa halmashauri ya jiji, wamepima viwanja kwenye eneo hilo wakishirikiana na wakazi ambao ilikuwa walipwe fidia kwa mashamba yao, na wakazi hao wanatumiwa kutafuta wateja wa viwanja hivyo ili ionekane wao ndiyo walioviuza kwa watu wanaojenga sasa.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla jana alitembelea eneo hilo lililopo Veta jijini Mbeya  na kujionea majengo yaliyojengwa kwenye ardhi, iliyokuwa sehemu ya uwanja wa kujengwa Ikulu ndogo ya Mkoa.

Diwani wa Kata ya Ilomba, Dickson Mwakilasa alimwambia Mkuu wa Mkoa kuwa eneo lilikojengwa nyumba za watu binafsi, lilikuwa la serikali na kilichotakiwa ni kulipa fidia kwa wakazi waliokuwa na mashamba maeneo ya jirani.

Kufuatia hali hiyo, Makalla alilazimika kuwahoji maofisa wa halmashauri ya jiji, lakini wote wakaonekana kutoijua vyema historia ya eneo hilo, hivyo ikamlazimu Mkuu huyo wa Mkoa kuahidi kufuatilia kwa haraka nyaraka husika.

Alisema anachotaka kujua ni ramani inayoonesha ukubwa wa eneo la awali; na pia matumizi yaliyopangwa, huku akisema anachojua yeye mpaka sasa ni kuwa maofisa ardhi wameuza kinyemela sehemu ya uwanja wa Ikulu ya Mkoa.
Previous
Next Post »