WANAWAKE WAFUGA NYUKI KUOKOA MISITU YA PUGU NA KAZIMZUMBWI . - Rhevan Media

WANAWAKE WAFUGA NYUKI KUOKOA MISITU YA PUGU NA KAZIMZUMBWI .



WANAWAKE wanaofuga nyuki wataokoa hekta 7,270 za misitu ya hifadhi ya Pugu na Kazimzumbwi, imefahamika.

Misitu hiyo, ambayo ni miongoni mwa Misitu ya Hifadhi 486 iliyopo nchini, imekuwa hatarini kutoweka kutokana na shughuli za kijamii hususan uvamizi wa mipaka na ukataji wa miti kwa ajili ya uchomaji mkaa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukifanywa na wananchi mbalimbali.

Meneja wa Misitu hiyo kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mathew Mwanuo, anasema kwamba, misitu hiyo iliyopo katika wilaya za Ilala mkoani Dar es Salaam na Kisarawe mkoani Pwani, imekuwa hatarini kutoweka licha ya jitihada za serikali za kukabiliana na wavamizi hao.
 Alicia (wa pili kulia), mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka Hispania, akiangalia sega la nyuki katika msitu wa Kazimzumbwi.

“Lakini sasa miradi hii ya ufugaji nyuki inayowahusisha wanawake wa Pugu na Kisarawe itakuwa mkombozi kwa sababu wananchi wenyewe wanahusishwa moja kwa moja na suala la ulinzi,” anasema Mwanuo wakati akiwaelekeza wageni kutoka taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) kutoka nchini Hispania waliotembelea miradi hiyo hivi karibuni.

Mwanuo anasema kwamba, ndani ya misitu hiyo ya hifadhi kuna jumla ya vikundi vinne vya akinamama vinavyojihusisha na ufugaji wa nyuki wa kisasa, ambapo viwili vinafadhiliwa na mradi wa Green Voices Tanzania na viwili vinafadhiliwa na TFS.
Anna Salado akiwa msituni kuangalia ufugaji wa nyuki kwenye hifadhi ya Pugu.


Previous
Next Post »