HATUA ya serikali kuzuia kurusha moja kwa moja mjadala wa vikao vya Bunge kama ilivyokuwa awali, bado inaumiza wananchi.
Safari
hii wananchi wametinga mahakamani na kwamba leo wamefika katika
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kufungua kesi ya kuitaka mahakama
hiyo kutengua agizo la serikali la kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya
Bunge.
Januari
mwaka huu, Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Michezo na
Sanaa alilieleza Bunge hatua ya kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya
chombo hicho kama ilivyokuwa awali.
Miongoni
mwa sababu alizotoa ni kwamba, serikali imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa
gharama katika kuendesha matangazo hayo pia watumishi wa umma kutumia
muda mwingi kuangalia Bunge badala ya kufanya kazi.
Hatua
ya serikali kuzuia kurusha matangazo hayo ya moja kwa moja imeibua
mjadala mkubwa kitaifa ambapo kada mbalimbali nchini zimekuwa zikipinga
hatua hiyo.
Katika
kesi iliyofunguliwa leo, ina walalamikaji 10 ambao ni Azizi Himbuka,
Perfect Mwasililwa, Rose Moshi, Penina Nkiya, Andrew Mandari, Hilda
Sigara, Juma Uloleulole, Kubra Manzi, Ray Kimbito na Ben-Rabiu Saanane.
Kesi
hiyo imesikilizwa na Profesa Ferdinand Wambari, Jaji Kiongozi katika
mahakama hiyo, na jaji mwengine katika kesi hiyo Sakieti Kihiyo, hata
hivyo hakuwepo mahakamani leo.
Washtakiwa
kwenye kesi hiyo ni Nape pamoja na George Masaju, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG) ambapo Abubakari Mrisho, ndio wakili wa upande wa
walalamikiwa.
Kwa
upande wa walalamikaji unasimamiwa na Peter Kibatala na Omari Msemo
ambao ni mawakili wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kesi
ya msingi iliyofunguliwa ni kuitaka mahakama kutengua uamuzi uliotolewa
na Nape ambaye aliwasilisha kauli ya serikali bungeni.
Walalamikaji
wanaitaka mahakama itangaze kuwa, Raia wa Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania wana haki ya kikatiba ya kujua majadiliano yanayoendelea
bungeni kwa mujibu wa ibara ya 18(B), (d) na 29 (1).
Pili
walalamikaji wamedai kuwa, serikali imekiuka haki ya kikatiba kwa
kuzuia bila kuwa na sababu za msingi haki ya wananchi kusikia
majadiliano ya Bunge kwa kuzuia kurusha matangazo ya moja kwa moja.
Tatu,
walalamikaji wameitaka mahakama kuilekeza Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kurejesha haki ya kikatiba ya wananchi kwa kurusha
matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.
Nne,
walalamikaji wamedai kuwa, matokeo ya kuzuia matangazo hayo ni kunyimwa
kwa haki za Watanzania kutokana na kushindwa kuwasimamia pia
kuwafuatilia wabunge na mwenendo wao bungeni.
Tano,
walalamikaji hao wamedai kuwa, sababu za kuzuia matangazo hayo
hazijitoshelezi hivyo Watanzania na walalamikaji wanayo haki ya kupata
taarifa ya vikao vya Bunge kwa maslahi ya taifa.
Hata
hivyo upande wa utetezi ulidai kuwa, walichelewa kupata taarifa ya
mashtaka hayo hivyo hawakupata muda wa kutosha wa kuaandaa majibu.
Kutokana na hivyo, mahakama iliuambia upande wa walalamikiwa kwamba,
watajibu mashtaka hayo 15 Julai siku ambayo kesi hiyo itatajwa.
Sign up here with your email