WAFANYABIASHARA WAHIMIZWA KUCHUKUA MASHINE ZA EFD. - Rhevan Media

WAFANYABIASHARA WAHIMIZWA KUCHUKUA MASHINE ZA EFD.


Na: Lilian Lundo - MAELEZO - Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kugawa Mashine za Kutunza Hesabu za Kodi za Kielektroniki (EFD) bila malipo kwa wafanyabiashara wa kati na wadogo.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Ashatu Kachwamba alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Neema William Mgaya juu ya mpango wa serikali kugawa mashine hizo Nchi nzima.

“Nia ya Serikali ni kusambaza mashine za EFD Nchi nzima lakini tumeanza na Mkoa wa Dar es Salaam ambapo jumla ya mashine 5,703 zinaendelea kugawiwa kwa wafanyabiashara wa kati na wale wadogo ambao mauzo ghafi yao ni kati ya shilingi milioni 14 mpaka milioni 20 kwa mwaka,” alifanunua Mhe. Ashatu.

Aliendelea kwa kusema kuwa, japo mashine hizo zimekuwa zikitolewa bure lakini wafanyabiashara hawafiki katika ofisi za TRA kuzichukua. Hivyo amewataka kundi hilo la wafanyabiashara kufika katika ofisi za TRA wanazolipia kodi katika Mikoa ya Ilala, Kinondoni au Temeke kuchukua mashine hizo, kwani ni wajibu wa kila mfanyabiashara kutumia mashine hizo katika mauzo ya kila siku.



Previous
Next Post »