Barua pepe
TAMASHA la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, linaloandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, limetoa tuzo ya pekee kwa mwanzilishi wa Vikundi vya Benki za Kijamii (Vicoba), anayejulikana kwa jina la George Swevetta kwa mchango wake wa kukuza na kuimarisha uchumi kwa watu nchini.
Pia tamasha hilo limetoa tuzo kwa marehemu, Ntimbanjayo Milinga, kwa jitihada zake za kuanzisha kijiji cha ujamaa cha kwanza cha Litoa wilayani Songea na kwa Dk Maria Kamm aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Weruweru kwa mchango wake wa kuimarisha dhana ya ujamaa na kujitegemea.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Penina Mlama alikabidhi tuzo hizo jana katika kilele cha tamasha hilo, huku akisisitiza viongozi wa kitaifa wa sasa kumuenzi Nyerere kwa sifa alizokuwa nazo.
Akimzungumzia mwanzilishi wa Vicoba, Profesa Mlama alisema mfumo wa Vicoba umekuwa ukitumika sana nchini baada ya kuingizwa rasmi mwaka 2000 ukianzia Zanzibar na umekuwa na manufaa makubwa kwa vikundi mbalimbali vya kiuchumi hususani vya wanawake.
“Baada ya Swevetta kuona mfumo huo umekubaliwa vyema Zanzibar ndipo alipohamia Bara na kwenda moja kwa moja Kisarawe, Ukonga, Songea, Lindi, Mtwara na katika wilaya ya Hai iliyoko mkoani Kilimanjaro,” alisema Profesa Mlama.
Alisema kwa sasa Vicoba imekuwa ndio nguzo kuu nchini kote na imekuwa na manufaa makubwa kuanzia ngazi ya familia na hiyo inaonesha wazi mwanzilishi huyo alikuwa na moyo na ari ya kuleta maedeleo kiuchumi.
Kuhusu marehemu Milinga alisema alikuwa mwanzilishi wa kijiji cha Litoa na alianza harakati hizo akiwa na miaka 21 ikiwa ni kuitikia wito wa Mwalimu Nyerere wa kuanzisha vijiji vya ujamaa na kujitegemea.
Alisema kijiji hicho kilifanikiwa sana na wakazi wa eneo hilo waliweza kuishi kwa upendo, wakifanya kazi pamoja na walipouza mazao waligawana sawasawa huku pia wakianzisha miradi mingine ya maendeleo.
Profesa Mlama alisema pia Dk Kamm amekuwa mfano mzuri wa kuwapa elimu watoto wa kike na tangu alipokuwa mkuu wa shule ya sekondari ya Weruweru huku akiwa na uwezo mkubwa wa kufanya mambo kwa ufasaha.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo ya kuanzisha Vicoba nchini, Swevetta aliwashauri wanaume nao kujiunga kwa wingi katika mfumo huo kwani umekuwa na manufaa na ni nguzo kubwa katika kuimarisha na kukuza uchumi kuanzia ngazi ya familia.
Alisema hivi sasa wanawake wanafanya mambo mengi ya maendeleo kutokana na kuingia kwa uaminifu katika mfumo huo wa kuweka na kukopa.
Sign up here with your email