WAKATI pangua pangua ya nafasi
za wakuu wa mikoa (RC) na wale wa wilaya (DC) ikiwa imekamilika juzi,
siri nzito imegubika kufuatia kutenguliwa kwa uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa
Mara, Magesa Mulongo kulikofanywa wiki iliyopita.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi
ya wananchi waliopiga simu chumba cha habari cha gazeti hili, walisema
miongoni mwa viongozi ambao hawakuwa na shaka kuwa wangeendelea na
nafasi zao ni Mulongo, hasa kwa kuwa alikuwa mchapakazi hodari.
“Sijui kwa kweli, huenda kwa vile Rais
John Magufuli ndiye mwenye vigezo, lakini kama ni cha uchapa kazi na
umri, nadhani huyu jamaa alikuwa anafiti kabisa, maana kila siku
unasikia anavyowajibika hadi mtu unasema hapa tuna kiongozi, lakini
kilichotokea kwa kweli siri nzito iko kwa mwenye nchi,” alisema Oscar
Nelson, aliyepiga simu kutoka mkoani Mara.
Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa
jina moja la Mwajuma, akipiga simu kutoka Mwanza, alisema ameshtushwa
sana na kuondolewa kazini kwa Mulongo, kwani alikuwa kiboko cha
wabadhirifu na watumishi wavivu katika ofisi za umma.
“Ninamfahamu vizuri, alikuwa hapa
Mwanza, kwa kweli kama ni kazi huyu ni mchapakazi, lakini mambo mengine
nadhani rais ndiye anajua nini sababu ya kuondolewa kwake,” alisema
mwanamama huyo.
Magesa Mulongo anakuwa mkuu wa mkoa wa
pili kuondolewa kwenye nafasi yake tangu Rais John Magufuli awateue na
kuwaapisha mapema mwaka huu. Wa kwanza alikuwa ni Anne Kilango Malecela,
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, aliyefutwa uteuzi kwa kile
kilichodaiwa kukubaliana na ripoti ya wasaidizi wake kuwa mkoa huo
haukuwa na watumishi hewa.
Sign up here with your email
