KITENDO cha Simba kudaiwa kumtwaa Patrick Kahemele kuwa Katibu Mkuu wao, kimeitikisa klabu ya Azam aliyokuwa akiitumikia kama Meneja na Mratibu Mkuu wa timu.
Kahemele anaelezwa alitemwa na Azam FC kwa sababu ambazo hazikuweza kuwekwa wazi na hivyo Simba kuamua kumchukua ili kuiongezea nguvu klabu hiyo kwa wakati huu inapojipanga kurejesha makali yake.
Habari kutoka ndani ya Azam, zinasema kuwa klabu hiyo imepokea kwa hisia tofauti juu ya Kahemele kutua Simba, ikihofia kuvujishwa kwa siri zao hasa zilizokuwa zikihusiana na mikakati ya ushindi na mambo mengineyo ya kimaendeleo kisoka.
Chanzo cha kuaminika ndani ya Azam kimelipasha BINGWA kuwa Kahemele ni miongoni mwa watu waliokuwa wakihusishwa katika mambo mbalimbali, kuanzia ya kiufundi, kiutawala, mikakati ya kuiboresha klabu hiyo na mengineyo mengi.
“Japo alitemwa, lakini ilivyofahamika kuwa Simba wanamchukua, tumeanza kupata hofu kwani anabeba siri zetu na kuzipeleka Simba,” alisema mtoa habari huyo ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini.
Aliongeza: “Kuna uwezekano wa kuondoka na wachezaji wetu, hilo halitusumbui kichwa kwani kama kuna atakaowapata, ni wale ambao hawana umuhimu kikosini, kwa mchezaji mwenye nafasi kikosini hawezi kuondoka Azam na kwenda Simba.”
Mbali ya Kahemele, Simba pia wameripotiwa kuwa katika mkakati kabambe wa kumtwaa aliyekuwa kocha wa zamani wa Azam, Joseph Omog ambaye ni raia wa Cameroon.
Tayari imeelezwa kuwa Simba wanajiandaa kumkabidhi Omog mikoba ya usajili wa wachezaji, hasa wa kimataifa ili kukisuka upya kikosi chao, akisaidiwa na Mganda, Jackson Mayanja.
Imedaiwa kuwa Omog anatarajia kuwasili nchini muda wowote kuanzia sasa kusaini mkataba, tayari kuanza rasmi kazi yake.
Simba imeangukia kwa Omog baada ya jitihada zao za kumnasa Mzimbabwe, Kalisto Pasuwa, aliyekuwa chaguo lao namba moja kushindikana kama ilivyokuwa kwa Mghana, Sellas Tetteh.
Sign up here with your email
