Katika fani ambayo mambo hugeuka haraka sana na tena kila
mwaka, nadhani uongozaji wa video unaongoza. Hii ni fani ambayo
aliyekuwa namba moja mwaka jana, mwaka unaofuata hawezi kubweteka tena,
infact taji lake huchukuliwa bila yeye mwenyewe kutarajia.
Wameshawahi kuja waongozaji wengi wa video nchini, wapo waliopotea kabisa na kuamua kubadilisha fani na wapo wanaoendelea kufanya kazi nzuri. Ningependa kwanza kusema kuwa hadi sasa ni muongozaji mmoja tu wa video ambaye anapewa ile title ya ‘hall of fame’ kwa mchango mkubwa alioufanya kwenye video za Tanzania. Naye si mwingine bali ni Adam Juma. Adam ni P-Funk au Master J kwenye video za Bongo kwahiyo heshima yake itabaki pale pale.
Lakini walikuja kuibuka waongozaji wengine miaka mitatu iliyopita ambao wamekuja kubadilisha kabisa upepo wa video za muziki. Mwaka 2014 ulikuwa mwaka wa Nisher hadi kupelekea kushinda tuzo ya muongozaji wa video anayependwa mwaka huu. Nisher alikuwa na hasira na mawazo mapya katika ufanyaji video. Video kama Nje ya Boksi, Jikubali, Nakomaa na Jiji na zingine zilionesha uwezo wa muongozaji huyu wa Arusha.
Nisher pia aliweza kuinspire vijana wengi waliopenda aina yake ya uchukuaji na umaliziaji wa video. Lakini kiti chake kilikuja kuchukuliwa mwaka 2015 na hasimu wake, Hanscana. Mwaka huo pia Hanscana alichukua tuzo ya muongozaji wa video anayependwa kwenye Tuzo za Watu. Video kama Nasema Nawe, Siri na zingine kibao, zilimpandisha chati na kumfanya kuwa muongozaji anayetafutwa sana. Mwaka huu pia Hanscana ameongoza video kali ikiwemo Fundi ya Mheshimiwa Temba na Kama Utanipenda ya Darassa na zingine.
Lakini mambo yamebadilika tena, na hakika mwaka huu ni wa muongozaji mwingine. Mwaka huu ni wa Msafiri aka Travellah wa kampuni ya Kwetu Studios. Msafiri si mgeni kwenye video za muziki wa Tanzania. Naamini amekuwepo hata kabla ya Nisher na Hanscana lakini hakufanikiwa kuwa mtu anayezungumzwa sana kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii kama wenzake.
Ameongoza video kibao za Hemed PHD na Jerry wa Rhymes na hapo mwanzo ilionekana kuwa wawili hawa ndio waliokuwa wanauelewa zaidi uwezo wake. Lakini mwaka huu, Msafiri – jiwe walilolikataa waashi, limegeuka mkate. Amekuja tofauti sana na kwa muda mfupi tayari amekuwa muongozaji wa video anayetafutwa zaidi.
Si kitu kilichotokea ghafla tu, lakini video zake mpya zina utofauti mkubwa.
Mwaka huu Msafiri amewashtua watu kwa video kibao kali zikiwemo Jike Shupa ya Nuh Mziwanda, Chafu Pozi ya Billnass, Pesa ya Madafu ya Jay Moe, Mboga Saba ya Mr Blue f/ Alikiba na zingine.
Ukiangalia video ya Mr Blue utagundua mabadiliko makubwa ya video zake kuanzia rangi, zinavyong’aa, uchukuaji picha na mengine.
Ni wazi kuwa Msafiri atakuwa ameboresha vitu vingi vikiwemo vifaa anavyotumia na hata ujuzi wake katika utengenezaji wa video. Naamini kuwa ana mengi ya kutushangaza siku za usoni na bila shaka anaingia kwenye orodha ya waongozaji muhimu wa Tanzania wanaohitaji kupewa support.
Sign up here with your email