DAR ES SALAAM: Katika kudhibiti
biashara ya usafirishaji wa madawa ya kulevya nchini, Marekani imeleta
mbwa wenye uwezo wa hali ya juu katika kutambua madawa ya kulevya na
nyara za serikali, ambao wamewekwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na viwanja vingine.
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege
nchini, ACP Martin Otieno aliliambia Risasi Mchanganyiko kuwa ukaguzi wa
mizigo ya wasafiri, bila kujali hadhi yao, hufanywa katika maeneo yote
yanayopitisha mizigo, kwa abiria wa kawaida na hata VIP.
“Hakuna exceptional (maalum), kila mtu
anakaguliwa, tuna mashine maalum pamoja na mbwa ambao tumepewa na
Marekani, wana uwezo wa kutambua aina zote za madawa na nyara, wanakagua
mizigo yote na watu wote hata wale wanaopita mlango wa watu mashuhuri
(VIP), wote wanakaguliwa,” alisema.
Kamanda Otieno alitoa kauli hiyo baada
ya kuulizwa kuhusu madai ya watu mashuhuri kutumika kusafirisha madawa
hayo yanayopigwa vita dunia nzima, kwa maelezo kuwa wao na mizigo yao,
haikaguliwi kwa sababu ya heshima na vyeo vyao.
“Hakuna mtu anapita hapa bila
kukaguliwa, hata viongozi, wao na mizigo yao yote lazima ikaguliwe, iwe
ni Waziri, Mbunge au kiongozi yeyote, mfanyabiashara mkubwa, kila mtu
hapa lazima apite kwenye mashine yeye na mizigo yake,” alisema Otieno.
Kumekuwa na madai ya muda mrefu kuwa
watu maarufu, hasa wasanii wamekuwa wakitumika kusafirisha madawa hayo
kwa kinachodaiwa kuwa wao hawakaguliwi.
Miaka michache iliyopita, Video Queen
Agnes Gerald ‘Masogange’ alikamatwa uwanja wa ndege jijini Johannesburg
nchini Afrika Kusini akiwa na aina mojawapo ya madawa ya kulevya
akitokea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ambako inadhaniwa alipita
bila kukaguliwa.
Sign up here with your email
