KIAMA KWA MAGAIDI SASA KUFUNGWA MAISHA , KIFO - Rhevan Media

KIAMA KWA MAGAIDI SASA KUFUNGWA MAISHA , KIFO

SERIKALI imeweka adhabu kwa makosa ya ugaidi kuwa ni kifo, kifungo cha maisha au kifungo cha miaka 30 jela.
Adhabu hizo zimeainishwa katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali uliowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju mwishoni mwa wiki.
Masaju alisema  sheria ya kuzuia ugaidi ilivyo sasa haitaji adhabu kwa mtu anayetenda makosa ya ugaidi.
“Muswada huu unapendekeza adhabu kwa makosa hayo iwe kifo iwapo tukio la ugaidi limesababisha kifo, kifungo cha maisha iwapo kosa husika limesababisha madhara makubwa kwa mtu au mali na adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa mazingira mengine,”alisema.
Mapendekezo hayo yalikubaliwa na Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba ambayo ilisema adhabu hiyo itadhibiti ipasavyo vitendo vya ugaidi ambavyo vimekuwa na athari kubwa kwa maisha ya watu na uchumi wa nchi kutokana na kuzorotesha amani.
Udhabu ya ujauzito
Serikali pia imebainisha adhabu kwa kwa anayempa ujauzito mwanafunzi wa shule ya msingi ama sekondari, kuoa au kuolewa na mwanafunzi na mwanafunzi kuoa mtu yeyote, ni kifungo cha miaka 30 jela.
“Kifungu namba 60 A kinapendekeza adhabu ya Sh milioni tano au kifungo cha miaka mitano gerezani au vyote kwa pamoja kwa mtu atakayebainika kusaidia, kushawishi au kufanikisha mwanafunzi wa shule ya msingi ama sekondari kuolewa au kuoa,”alisema AG.
Awali adhabu kwa makosa ya kumpa ujauzito mwanafunzi ilikuwa faini isiyozidi Sh 500,000 na kosa la pili   faini Sh 500,000 au jela miaka mitatu.
Kamati ilikubaliana na mabadiliko hayo na kuongeza kwamba yanalenga kumjengea mwanafunzi wigo wa ulinzi na mazingira mazuri ya kumwezesha akamilishe masomo yake kwa ngazi hizo.
Muswada huo unatarajia kumaliziwa kujadiliwa leo na baadaye kupitishwa endapo wabunge watakubaliana.
Previous
Next Post »