BREAKING NEWS : WAZIRI WA JK AMVAA MAGUFULI. - Rhevan Media

BREAKING NEWS : WAZIRI WA JK AMVAA MAGUFULI.


Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
ALIYEKUWA Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Serikali ya awamu ya nne, Dk. Makongoro Mahanga amesema kura milioni sita za Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (Chadema),  zilizopatikana kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ndizo zinazoiogopesha serikali ya Rais Dk. John Magufuli  na chama tawala.
Makongo ambaye alikuwa Naibu Waziri katika Serikali ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, amesema   hali ya ukandamizwaji wa demokrani nchini si ya kufumbiwa macho na Watanzania kutokana na kile alichodai ni ukandamizaji dhidi ya demokrasia.
“Mwaka 1992 serikali ilikubali kuingiza mfumo wa vyama vingi nchini katika Katiba na baadaye walitunga sheria kusimamia hilo na waliopitisha jambo hili kwa asilimia 100 walikuwa ni wabunge wa CCM.
“Leo hii nashangaa wanakipinga kile walichokikubali. Wanavizuia vyama visifanye siasa wakati Katiba imeruhusu, sijui walikuwa wanafikiria nini wakati ule, kwamba havitakuja kukua na kisha kuchukua nafasi!
“Kwa msingi huu ni wazi kwamba CCM inajuta kupitisha jambo lile na kinachowaogopesha hadi kuchukua uamuzi tunaouona leo, ni zile kura milioni sita za upinzani… zimewashtua kwamba tunakoelekea watachukua madaraka ya kuongoza nchi,” alisema.
Alisema   sasa ni wazi kuwa upinzani umekaribia kushika dola kwani hata wananchi wameichoka   CCM.
“Niliona dalili hizo na nilisoma nyakati ndiyo maana nilichukua uamuzi wa kukihama mapema. Lakini nashangaa kwa nini kama hawataki vyama vingi wasirudi bungeni na kukiondoa kipengele hicho kwenye Katiba   tujue kwamba tunafanya siasa za mchezo.
“Ila wasipoondoka ni wazi kwamba tunaelekea kushika dola baadaye,” alisema.
Dk. Mahanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, alisema Rais Magufuli anapaswa kukumbuka ahadi aliyoitoa wakati akiapishwa, ya kuilinda Katiba ya nchi.
“Rais Magufuli ni rafiki yangu wa muda mrefu tangu kule chuoni, wakati wa kampeni alitoa ahadi nyingi lakini  kuu ni mbili.
“Moja ni kuilinda Katiba na pili kupeleka maendeleo kwa wananchi, lakini amekuwa hataji hii ya kuilinda Katiba kwenye mikutano yake na kutaja ile ya maendeleo peke yake.
“Anachokifanya ni wazi kuwa anavunja Katiba ya nchi kwa sababu ndani yake kuna suala la kulinda demokrasia. Namshauri akumbuke ahadi hii ya kuilinda Katiba vinginevyo tunapokwenda ni kubaya,” alisema.
Naye  Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alisema chama hicho kimeridhia viongozi wake wote kutohudhuria mikutano yote atakayohudhuria Rais Magufuli.
“Alihoji kwa nini mameya hawakuhudhuria Biafra, kwanza mwaliko ule ulichelewa kufikishwa ofisini lakini tumekubaliana pia kufanya hivyo   kuwalinda mameya wetu kwa vile umekuwako  ubaguzi na udhalilishaji wa wazi katika baadhi ya hafla ambazo walihudhuria,” alisema.
Awali akisoma tamko hilo, Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Casimir Mabinam, alisema Rais Magufuli anapaswa kutengua kauli yake aliyoitoa ya kuzuia siasa hadi 2020 kwa sababu  inakandamiza upinzani nchini.
Previous
Next Post »