Yassin alisema tangu sasa ni muhimu kila ofisa tarafa kupeleka taarifa ya hali halisi ya tarafa yake kila wiki wakieleza pia namna wanavyotekeleza majukumu yao ikiwamo kutatua kero za wananchi katika maeneo yao.
Aliwaambia kwamba kero zilizo nje ya uwezo wao wazifikishe kwake ili aone namna ya kuzitatua huku akisisitiza kwamba kazi yao kubwa ni kuwatumikia wananchi. Mkuu huyo wa Wilaya aliwaeleza maofisa tarafa hao kwamba, kwa sasa kazi kubwa ni kuwahimiza watu kufanya kazi hasa vijana na kwamba hivi karibuni ataanza ziara za kutembelea vijiji vyote vya Makete ili kuonana na wananchi, lakini pia kuona shughuli wanazofanya na kusikiliza kero zao.
“Tufanye kazi kwa bidii, kila mmoja atimize wajibu wake,” alisisitiza. Wananchi wanachotaka ni kupiga hatua mbele za maendeleo. Katika kikao hicho, pia alikuwepo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Makete, Francis Namaumbo ambaye alihimiza mshikamano katika utekelezaji wa majukumu na uadilifu.
Maofisa Tarafa hao walimwahidi Mkuu wa Wilaya kwamba wataendelea kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa kanuni na sheria, watatekeleza maagizo yote waliyopewa ikiwamo kuhakikisha hali ya utulivu na amani, inaendelea kuwapo wilayani Makete.
Sign up here with your email
