CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetangaza kuitisha Mkutano Mkuu wa Taifa
kwa ajili ya kujaza nafasi za uongozi zilizo wazi ikiwemo nafasi ya
Uenyekiti iliyokuwa inashikiliwa na Profesa Ibrahim Lipumba.Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema chama hicho kimeitisha mkutano huo mkuu wa taifa Agosti 21, mwaka huu kwa lengo la kukiimarisha tayari kwa kuanza mapambano ya kuwapigania wananchi wa taifa hili.
Mketo alisema kuitishwa kwa Mkutano Mkuu kumetokana na kuwa wazi kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa kutokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Lipumba, Agosti 5, 2015.
Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa CUF kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kusutwa na dhamira yake baada ya chama hicho kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kumteua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea urais.
Lowassa aliteuliwa na Chadema kuwania nafasi hiyo na akaungwa mkono na CUF, NCCR Mageuzi na NLD. Hata hivyo, hatua hiyo haikumfurahisha Lipumba akatangaza kuachia wadhifa huo na kwa upande wa Chadema aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Dk Willbrod Slaa naye alitangaza kujiuzulu wadhifa huo.
Mketo alisema mkutano mkuu huo pia umeitishwa ili kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti baada ya aliyekuwa anashikilia wadhifa huo, Juma Duni Haji kuamua kujiuzulu na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Duni alijiunga Chadema na hatimaye kuteuliwa kuwa mgombea Mwenza ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho na hivyo kupoteza sifa za kuwa kiongozi wa CUF. Hivi karibuni amerejea CUF.
Mketo alisema zipo pia nafasi nne za wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ambazo nazo zinapaswa kujazwa ambazo ni nafasi moja ya mjumbe kutoka Kanda ya Kusini, nafasi moja ya Mjumbe kutoka Kanda ya Kati, nafasi moja ya mjumbe kutoka Kanda ya Kaskazini na nafasi moja ya Mjumbe mwanamke kutoka Kanda ya Ziwa.
Mketo alisema fomu za kuomba uongozi zitapatika katika ofisi za makatibu wa wilaya zote nchini na kwamba ada za malipo ya nafasi za uongozi ni kama zilivyo katika Kanuni ya Uchaguzi ndani chama ya mwaka 2014. Fomu zitaanza kuchukuliwa Julai mosi hadi Julai 20, mwaka huu.
Sign up here with your email
