Kijana Lucas John alivyokatwa mguu.
Na Dege Masoli, UWAZI
TANGA: Kijana Lucas John (32)
anayeishi Kijiji cha Ngombezi, wilayani Korogwe, Mkoa wa Tanga,
anaugulia maumivu nyumbani kwao akiwa kitandani baada ya kupata ulemavu
wa kudumu kwa kukatwa miguu na mkono wake wa kulia na watu
wasiojulikana.
Kabla ya kukumbwa na mkasa huo, kijana
huyo ambaye ni mlemavu na mwenye kuzungumza kwa shida kutokana na
kushindwa kutamka maneno vyema, alizoeleka kuonekana mitaani Korogwe
mjini akiomba fedha kwa wasamaria wema zilizosaidia familia yake
kujikimu.
Mama wa kijana huyo, Herieth Mndolwa
alilielezea Uwazi kwamba Lucas ni yatima baba yake alifariki kwa ajali
na hivyo kulazimika kuishi naye katika mazingira magumu baada ya
kutokuwa na kazi wala kipato cha kuwawezesha kupata mlo wa kila siku.
Alisema kuwa mwanawe alitoweka nyumbani
tangu Mei 4, mwaka huu, hali iliyompa wasiwasi kutokana na ukweli kuwa
haikuwa kawaida ya Lucas kutokurejea nyumbani kwao hatua iliyosababisha
kutaka kujua alikokwenda.
Katika jitihada za kujua ni wapi kijana
wake alielekea, Herieth alisema kwamba alilazimika kuomba msaada katika
Kanisa la Pentekoste anakosali ili kumuombea kwa Mungu ambapo ibada
ilifanyika na siku chache baadaye ndipo alipofanikiwa kupata taarifa juu
ya kijana wake huyo.
Hata hivyo, mama huyo ambaye tukio hilo
analihusisha na imani za kishirikina alieleza kuwa alipata taarifa za
kijana wake huyo kuwepo Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo na
kulazimika kwenda kumuona na kudai kuwa alimkuta akiwa amekatwa mkono
wa kulia, mguu wa kushoto na unyayo wa kulia.
Kwa mujibu wa mama huyo, baada ya
kumkuta mwanaye katika hali hiyo alilazimika kwenda polisi kujua
kilichojiri na kueleza kuwa taarifa alizozipata polisi zinadai
kuwa kijana huyo aligonga treni na kwamba aliokotwa relini kauli ambayo
ilimuumiza sana na kuacha maswali kwake.
Kutokana na taarifa hizo aliamua kudai
viungo vya mwanaye lakini polisi walimjibu kuwa vilibebwa na kunguru
jambo ambalo hakukubaliana nalo na kutaka apewe maelezo zaidi kuhusiana
na viungo hivyo.
“Polisi waliniambia mama usijaribu
kufuatilia tukio hili ni baya kwani mwanao amegonga treni na
kisheria anatakiwa kushitakiwa kwa kuligonga treni na wakanishauri
niondoke kabla sijakamatwa, nikakimbilia nyumbani bila kupata viungo vya
mwanangu,” alisema Herieth.
Aidha, aliongeza kuwa utata mwingine ni
wa maelezo ya Lucas ambayo yanapingana na taarifa ya polisi ya kupata
ajali na badala yake anaeleza kuwa alikatwa viungo hivyo na watu huku
akimtaja kwa jina mmoja wao na jinsi alivyomfikisha katika eneo la tukio
alikookotwa.
Herieth anaomba msaada wa serikali,
taasisi na wasamaria wema wenye moyo wa kusaidia kutokana na mateso
anayoyapata Lucas ambayo yanachangiwa na umaskini wake ili kumpatia
matibabu kwani kila siku analazimika kusafirishwa hadi Hospitali ya
Wilaya Magunga kwa matibabu baada ya kuruhusiwa Bombo.
“Mimi siamini kama mwanangu amekatwa
viungo na treni kwa sababu hakuna mguu wala mkono uliookotwa, kunguru
gani anaweza kubeba mguu na mkono? Mbona mtoto anawataja watu waliomkata
na kwenda kumtupa relini?” alihoji mama huyo.
Kijana huyo alisema alichukuliwa na mtu
Hale wilayani Korogwe na kusafiri naye hadi Tanga Mjini kwa pikipiki
ambapo baada ya kumfanyia unyama huo, mtu huyo akiwa na
mwenzake walimtelekeza relini.
Lucas anaomba msaada kwa kuwa maisha
anayoishi ni magumu na anakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo
matibabu na kujikimu kimaisha kwani mama yake hawezi majukumu hayo
kutokana na kutokuwa na uwezo.
Sign up here with your email
