Tanzania inatarajia kuanza kuzalisha umeme wa jotoardhi zaidi ya
megawati 20 ifikapo mwaka 2018 mradi utakaopunguza gharama za nishati
hiyo nchini.
Kiwango cha nishati hiyo kitakachozalishwa kutoka
miradi minne inayoendelea kufanyiwa kazi kwa sasa, kinatarajiwa
kuongezeka mpaka megawati 200 ifikapo mwaka 2025.
Mkurugenzi wa
Kampuni ya Jotoardhi nchini (TGDC), Mhandisi Boniface Njombe aliwaeleza
wajumbe wa mkutano wa wataalamu wa jotoardhi jana kuwa, mbali na mpango
huo wa muda mfupi, wamejiwekea malengo ya kuzalisha zaidi ya megawati
200 ndani ya miaka tisa ijayo.
“Hii ni nishati salama na rafiki
wa mazingira,” alieleza bosi huyo wa TGDC ambayo ni kampuni tanzu ya
Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco).
Mpaka sasa miradi
inayoendelea kufanyiwa kazi ikiwa kwenye hatua mbalimbali ni Ngozi na
Mbaka iliyopo mkoani Mbeya, Kisaki wa Morogoro, Mlima Meru na Ziwa
Natron kwenye Mlima Lengai.
Alisema, TGDC inashirikiana na
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira (UNEP) kufanya
mapitio ya jotoardhi, kuendeleza na kuchakata nishati hiyo kabla
haijaanza kutumika.
Akifungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Dk Juliana Pallangyo alisema Tanzania ina
hazina ya takriban megawati 5,000 ya nguvu za kuzalisha nishati hiyo na
kwamba ipo karibuni kuanza kuitumia.
Alisema mpango wa Serikali
ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na utafikiwa endapo kutakuwa
na nishati ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani na viwandani.
Sign up here with your email