SERIKALI IMESEMA IMESHTUSWA NA WIMBI KUBWA LA VIJANA WA KITANZANIA WANAOJIUNGA NA MAKUNDI HATARI YA KIGAIDI YA AL-SHABAABA NA ISLAMIC STATE , MAARUFU KAMA ISIS. - Rhevan Media

SERIKALI IMESEMA IMESHTUSWA NA WIMBI KUBWA LA VIJANA WA KITANZANIA WANAOJIUNGA NA MAKUNDI HATARI YA KIGAIDI YA AL-SHABAABA NA ISLAMIC STATE , MAARUFU KAMA ISIS.

SERIKALI imesema imeshtushwa na wimbi kubwa la vijana wa Kitanzania wanaojiunga na makundi hatari ya kigaidi ya Al-Shabaab na Islamic State, maarufu kama ISIS.

Kauli hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake ya Sh trilioni 1.6 kwa mwaka 2016/17.

Dk. Mwinyi alisema pamoja na hali hiyo, Serikali imeendelea kupambana na makundi hayo kwa kila njia ili kuhakikisha nchi inakuwa salama katika maeneo yote, yakiwamo ya mipakani.

Alisema matukio ya kigaidi yameendelea kuwa tishio duniani, hivyo Tanzania inapaswa kuchukua tahadhari ya kila namna.

Dk. Mwinyi alisema kuwapo kwa makundi hayo ya Al-Shabaab, Al-Qaeda, Boko Haram na Islamic State, kunafanya tishio la ugaidi kusambaa duniani kote.

“Taarifa za kuwapo baadhi ya Watanzania wanaojiunga na makundi ya Al-Shabaab na ISIS tunazo, kunahatarisha usalama wa Tanzania, hasa ikizingatiwa kiujumla mwingiliano mkubwa uliopo kati ya wananchi wetu na watu wenye malengo tofauti.

“Hatari iliyopo ni uwezekano wa baadhi ya vijana waliojiunga na makundi ya kigaidi ya kimataifa kurejea nyumbani kwa lengo la kutekeleza vitendo vya kigaidi nchini mwetu.

“Tuna kila sababu ya kujizatiti na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama,” alisema Dk. Mwinyi.

Alisema kipindi kilichopita, kumejitokeza viashiria vyenye mwelekeo wa kigaidi, ikiwemo kuvamiwa baadhi ya vituo vya polisi, kuporwa silaha na baadhi ya askari kuuawa na kundi ambalo nia yake haijafahamika.

“Matukio yenye mwelekeo wa kigaidi, ni kama yaliyotokea katika mapango ya Amboni mkoani Tanga, Kitongoji cha Nyandeo wilayani Kilombero pale Morogoro na kukamatwa mabomu ya kutengenezwa kwa mkono katika maeneo mbalimbali yakiwamo Zanzibar,” alisema.

Alisema pamoja na hali hiyo, kwa upande wa mpaka wa kusini mwa nchi, hali imeendelea kuwa shwari, licha ya uwapo wa utata wa mpaka wa Ziwa Nyasa ambao bado haujapatiwa suluhisho.

Kutokana na hali hiyo, amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kwa kutoa taarifa ya matukio yanayotishia kuashiria uvunjifu wa usalama.

Kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana na ule wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu Zanzibar, alisema umefanyika kwa amani na utulivu, licha ya baadhi ya maadui wa ndani na nje kutabiri mambo mabaya.

“Watanzania tunayo sababu ya kujivunia kuwa uchaguzi mkuu ambao kikalenda ni wa tano tangu kuingia mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, uliendeshwa na kuhitimishwa kwa amani, utulivu na mshikamano mkubwa kinyume na maadui wetu wa ndani na nje ya nchi waliotutabiria mabaya,” alisema.
Previous
Next Post »