GGM NA TACAIDS WAMTEUA MRISHO MPOTO KUWA BALOZI WA KILI CHALLENGE. - Rhevan Media

GGM NA TACAIDS WAMTEUA MRISHO MPOTO KUWA BALOZI WA KILI CHALLENGE.

Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya kupambana na Ukimwi nchini (TACAIDS) imemteua msanii maarufu Mrisho Mpoto kuwa balozi wa kampeni ya Kili Challenge.

Kili Chalenge ni kampeni inayolenga kukusanya fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko wa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI. Kampeni hiyo ilianzishwa miaka 15 iliyopita na hufanyika kila mwaka kwa wadau mbalimbali kupanda mlima Kilimanjaro.Mwaka uliopita 2015 watu 39 walifanikiwa kupanda Mlima na kuchangisha fedha zaidi ya Sh bilioni 1.2  ambazo zitagawiwa kwa Asasi mbalimbali tarehe 20 Mwezi huu pale Hyatt Regency Dar es Salaam,Mgeni rasmi atakuwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Mrisho Mpoto ameteuliwa kuiwakilisha na kuitangaza kampeni hii ili kusaidiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kupambana na janga hili la Taifa. Mrisho Mpoto anakuwa Balozi mpya katika Kampeni hii kwa sababu ni msanii mwenye ushawishi ndani ya jamii na kupitia kazi zake za kisanaa tunaamini ataweza kuihamasisha jamii ipasavyo kuona umuhimu wa kumaliza tatizo la VVU na UKIMWI hasa katika masuala ya unyanyapaa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Fatma Mrisho, “Inakadiriwa kuwa watu milioni 1.6 nchini wanaishi na VVU & Ukimwi. Ugonjwa huo umewaathiri zaidi vijana na watoto yatima zaidi ya milioni 1.3. Tunahitaji kubadilisha hali hii.  TACAIDS kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na wadau wengine kwa kupitia mpango huu wa Kilimanjaro Challenge tunapenda kutoa mchango na ushirikiano wetu kwa Taifa ili kutunisha mfuko utakaowezesha kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo”.

Napenda kuupongeza  Mgodi wa Dhahabu wa Geita kwa kushirikiana na wadau wengine kwa kuamua kwa dhati kwa kipindi cha miaka 15 kuwekeza katika mradi huu kwa kuuwezesha kuwa mradi wa kitaifa na si wa GGM, hivyo pamoja na balozi wetu hivi sasa Mrisho Mpoto,  tuungane nao ili kuongeza chachu kwa wadau wengine kujitokeza kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya janga hili” alisisitiza Dkt Fatma Mrisho.

Previous
Next Post »