MANJI AUNDIWA ZENGWE YANGA , VIGOGO WAWILI WAANDALIWA.. - Rhevan Media

MANJI AUNDIWA ZENGWE YANGA , VIGOGO WAWILI WAANDALIWA..

SIKU chache baada ya Yanga kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu huku ikiwa bado na mechi mbili mkononi, hali ya hewa imeanza kuchafuka ndani ya klabu hiyo.
Imebainika kuwa hivi sasa kuna mpango kabambe unaoendeshwa chini kwa chini na vigogo wawili ambao mmoja wao amewahi kushika nafasi kubwa serikalini kwa lengo la kutaka  kumuangusha,  Yusufu Manji ambaye ndiye mwenyekiti wa Yanga hivi sasa katika uchaguzi mkuu ujao wa klabu hiyo.
 

Uchaguzi Mkuu wa Yanga umepangwa kufanyika Juni 27, mwaka huu baada ya kukamilika kwa taratibu zote za zoezi hilo na Manji anatarajia kutetea kiti chake hicho.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo Championi Jumatano limezipata zimedai kuwa, vigogo hao wamefikia hatua hiyo kutokana na kile wanachodai kuwa ni kutoridhishwa na utendaji kazi wa Manji.
 

 “Hilo ndilo lililopo hivi sasa hapa Yanga ambapo vigogo hao ambao mmoja kati yao amewahi kushika nafasi kubwa serikalini wanataka Manji aondoke ili wao wamuweke mtu wao ambaye wanaona kuwa atafaa kuiongoza Yanga ambaye tayari wameshamuandaa.
 

“Pia hivi sasa wanaendelea na kampeni ya kuwashawishi baadhi ya wanachama lakini pia wana mpango wa kutaka kukutana na wadhamini wa Yanga ambao ni Mama (Fatuma) Karume, Mzee Francis Kifukwe na Abass Mtemvu ili waweza kuwaunga mkono katika hilo.
 

 “Hata hivyo sidhani kama watafanikiwa kuwashawishi wadhamini hao wa Yanga kwa sababu wanamkubali sana Manji kutokana na makubwa aliyoifanyia Yanga tangu alipochaguliwa kuwa mwenyekiti,” kilisema chanzo hicho cha habari na kuongeza:
 

“Hali hiyo pia imeishtua TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kwani vigogo hao wawili wanaotaka kumwondoa Manji klabuni hapo, pia wana ushawishi mkubwa.
“Sasa ili kuondoa utata unaoweza kujitokeza, TFF imeamua kujiweka pembeni huku ikisubiria tarehe hiyo ya uchaguzi ifike na viongozi waweze kupatikana kwa kufuata kanuni na taratibu za katiba ya Yanga,” kilisema chanzo chetu.
Alipotafutwa Manji ili aweze kulizunguzia suala hilo hakuweza kupatikana.

Previous
Next Post »