Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imewapandisha kizimbani maafisa wawili, mmoja kutoka mamlaka ya mapato Tanzania TRA Bw. Amani Simson Mkwizu na mwingine wa Yono Action Mart Edward Magobela wakituhumiwa kwa mashtaka matatu ya kuomba rushwa ya fedha.
Washtakiwa hao wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu mbele ya hakimu Huruma Shahidi ambapo wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wakili Denis Lekayo akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo amedai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo april 19 mwaka huu.
Katika shtaka la kwanza mahakama imeambiwa kuwa washtakiwa hao walishawishi rushwa ya shilingi milioni 50, shtaka la pili walishawishi rushwa ya shilingi milioni 5 na shtaka la tatu kupokea rushwa ya shilingi milioni 3 kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Commercial, sells and services Tanzania limited Bw. Glenk Clerk ambapo wastakiwa hao walikuwa na lengo la kupunguza gharama za ulipaji kodi kutoka kiasi cha shilingi milioni 375 hadi milioni 100 toka kampuni hiyo.
Hata hivyo washtakiwa wote hao kwa nyakati tofauti walikana mashtaka hayo ambapo hadi ITV inaondoka mahakamani hapo dhamana kwa Washtakiwa hao zilikuwa wazi na walikuwa wakihangaikia dhamana zao.kesi hiyo itatajwa tena Mei 9 mwaka huu.
Sign up here with your email