WAWEKEZAJI WA NDANI WATAKIWA KUJIAMINI. - Rhevan Media

WAWEKEZAJI WA NDANI WATAKIWA KUJIAMINI.




Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania, Mhandisi Ray Ywa Seng’enge (kushoto) akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kabla ya kuanza kwa kikao hicho.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akifafanua jambo kwa ujumbe kutoka Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania ofisini kwake mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania uliomtembelea ofisini kwake. 


Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amewataka wawekezaji nchini kujiamini na kuwekeza katika sekta za Nishati na Madini ili sekta hizo zitoe mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Profesa Muhongo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika kikao chake na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania, Mhandisi Ray Ywa Seng’enge aliyeambatana na ujumbe wake. Kikao hicho kilishirikisha watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).

Profesa Muhongo alisema kuwa umefika wakati wa watanzania wenye uwezo katika uwekezaji hususan katika uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini kujitokeza na kuomba kazi kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kufanya kazi kwa ufanisi kwani uwezo wanao.

Alisema kuwa wawekezaji wengi wamekuwa na mtizamo hasi kuwa makampuni ya kigeni pekee ndiyo yenye uwezo wa kuzalisha na kusambaza umeme vijijini.

“Nataka niwahakikishie kuwa kampuni za kitanzania zina uwezo mkubwa katika uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini, na kama Serikali tupo tayari kuwasaidia ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema Profesa Muhongo.

Aliendelea kusema kuwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini ya REA awamu ya pili, zipo kampuni za kitanzania zilizoonesha uwezo katika miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme vijijini.

Akielekea mikakati ya Serikali ya kuwajengea uwezo wawekezaji wadogo wazawa Profesa Muhongo alieleza kuwa kampuni za kitanzania zimeonekana kujifunza kutokana na ushirikiano kati yao na kampuni za kigeni kwenye miradi ya umeme.

Awali akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania, Mhandisi Ray Ywa Seng’enge alimpongeza Profesa Muhongo na kuelezea shughuli zinazofanywa na chama hicho.

Akielezea mafanikio ya chama hicho Seng’enge alisema kuwa chama kimekuwa kikitoa huduma Serikalini na makampuni binafsi ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya uhandisi.

Alisema kuwa wakiwa na kampuni ya ushauri katika masuala ya uhandisi, wamekuwa wakishirikiana na makampuni mengine yaliyopo nje ya nchi.

Akielezea changamoto katika utendaji wa kampuni hiyo Seng’enge alisema kuwa kampuni yao imekuwa ikitumiwa zaidi na makampuni yaliyopo nje ya nchi katika utoaji wa huduma na kuiomba Serikali kuwasaidia na kuahidi kutoa ushirikiano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Previous
Next Post »