WATUMIAJI SIMU FEKI WAANZA KUHAHA WAILILIA TCRA. - Rhevan Media

WATUMIAJI SIMU FEKI WAANZA KUHAHA WAILILIA TCRA.

WAKATI Juni 17, mwaka huu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikitarajia kuzima simu zote feki, watumiaji wengi wa simu za mkononi nchini hawajui nini la kufanya na wamekumbwa na hofu ya kupoteza mawasiliano.

Idadi kubwa ya watumiaji wa simu za mkononi hususan wanaoishi maeneo ya vijijini bado hawajapata taarifa kuhusiana na suala hili na utekelezaji wake, hivyo mchakato huo utakapofanyika utawaacha bila mawasiliano.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti watumiaji wa simu hizo, walisema bado kuna haja ya muda kuongezwa huku elimu ikitolewa zaidi vijijini kwani wanaponunua simu huambiwa ni ‘orijino’ kumbe ni feki.
Kisamo Abdul wa Babati, Manyara alisema mbali ya watumiaji wengi ambao hawajapata taarifa juu ya suala hilo, vile vile wapo baadhi ambao wamesikia tangazo, lakini wanahitaji muda kufuatilia simu zao kama ni feki na wanaishi vijijini, hivyo watajikuta wanazimiwa simu zao kutokana na kutojiandaa.
“Kadhalika maisha ya Watanzania wengi hususan vijijini, hali zao ni duni, hivyo wanahitaji muda kujipanga zaidi ili kutoachwa nje ya mawasiliano, hivyo kuendelea kupata huduma ya kurahisisha maisha yao waliyozoea,” alisema.
Joyce Tarimo wa Tengeru, Arusha alisema: “Wengi wetu tunatumia simu hizi feki, hivyo kabla ya TCRA kuzizima, inapaswa kuzuia uingizwaji wake kwanza na kuhakikisha bidhaa hizo feki hazipo madukani na ndipo wazizime.”
Alisema sekta ya mawasiliano ya simu imekuwa ikiendelea kukua kwa kasi na kwamba taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano zinaonyesha kuwa laini za simu zilizouzwa na makampuni ya simu zimeongezeka kutoka milioni 2.1 zilizokuwapo mwaka 2004 na kufikia milioni 17.6 mwaka 2009 na hadi mwaka jana zimeongezeka kufikia milioni 28.
Alifafanua kuwa ongezeko hilo linadhihirisha kuwa karibia zaidi ya nusu ya Watanzania kwa sasa wanatumia simu za mkononi kwa maneno mengine wameingia katika ulimwengu wa mtandao.
Kadhalika, alisema ubunifu wa huduma mbalimbali uliofanywa na makampuni ya simu kwa sasa unaonyesga simu za mkononi si chombo cha kuongea tu bali zina matumizi mengi mojawapo ikiwa ni huduma za kifedha ambayo imerahisisha maisha vijijini huku wakizitumia pia kuhifadhi pesa zao.
Ramadhani Daudi wa Monduli, Arusha alisema kuna haja ya muda kuongezwa kwani watumiaji kunufaika kwa kurahishiwa maisha kupitia mawasiliano ya simu pia kuna ushahidi kuwa sekta hii imekuwa ikichangia mapato makubwa kwa serikali kupitia kodi mbalimbali zinazolipwa na makampuni yanayotoa huduma ya mawasiliano.
“Kwa mantiki hizi kuna umuhimu mkubwa kwa serikali na makampuni yanayotoa huduma za simu kuangalia madhara watakayoyapata watumiaji wengi wa simu wakati zitakapozimwa badala ya kulichukulia suala hili kama jambo dogo na kuwa na dhana kwamba mawasiliano ni anasa,” alisema.
“Japo sababu zinazosababisha simu kuzimwa zilizobainishwa na TCRA ni za msingi na zimedhamiria kuongeza ubora katika utoaji wa huduma za mawasiliano nchini sambamba na kutekeleza sheria za kimataifa, kuna umuhimu wa kutathmini na kujua kwa nini simu feki zipo nchini na kwa nini zinatumiwa na Watanzania wengi, alisema.
“Kwa nini ziliingizwa nchini wakati kuna vyombo vya kudhibiti viwango vya ubora wa bidhaa na ni kwa nini mbali na simu kuna bidhaa feki za aina mbalimbali zimejaa kwenye masoko?” alihoji.
Alisema jibu la maswali hayo mbali na matatizo ya kimfumo ni kuwapo na idadi kubwa ya Watanzania ambao hawana uwezo wa kumudu kununua simu na vifaa vinginevyo vyenye ubora unaotakiwa kutokana na makampuni yanayotengeneza bidhaa hizo kulenga soko la watu wenye vipato vya juu na kuuzwa kwa bei kubwa.
Alifafanua kuwa udogo wa vipato vya wananchi ambao wengi wanaishi chini ya matumizi ya dola moja kwa siku, umekuwa ukisababisha wananchi kutafuta bidhaa za bei ya chini ambazo nyingi ni feki ambazo wamekuwa wakizitumia kwa muda mfupi na bidhaa hizo kuharibika, lakini zikiwa zimewawezesha kupata huduma zinazorahisisha maisha yao kwa muda.
Alisema wakati zoezi hilo ambalo sio geni kufanyika katika nchi mbalimbali barani Afrika likikaribia kutekelezwa, serikali inapaswa kushirikiana na wadau wote kwenye sekta ya mawasililiano kujua jinsi gani ya kuhakikisha vinapatikana vifaa vyenye ubora unaotakiwa hususan simu.
Pia, serikali iangalie uwezekano wa kuongeza muda wa utekelezaji wa mchakato huo ili kutoa muda wa kutosha kwa wadau wa mawasiliano kujiandaa na kuingiza kwenye masoko bidhaa bora na zenye unafuu wa bei kama ambavyo nchi nyingine zimekuwa zikifanya.
Previous
Next Post »