WASOMI WAMJAJI MAGUFULI STAILI YA UTEUZI WA MA DC. - Rhevan Media

WASOMI WAMJAJI MAGUFULI STAILI YA UTEUZI WA MA DC.


BAADA ya Rais John Magufuli, kuja na mtindo wa kuteua wakuu wa wilaya mmoja mmoja kujaza nafasi zilizo wazi badala ya kufanya mabadiliko kwa nchi nzima, baadhi ya wasomi wamepongeza hatua hiyo wakisema inasaidia kubana bajeti na kupata watu makini.

Hivi Karibuni, Rais Magufuli alimteua, Gelasius Byakanwa, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kabla ya juzi kumteua Ally Hapi, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na Humphrey Polepole kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma.
Hatua hiyo ni tofauti na ya Marais waliotangulia ambao mara baada ya kuapishwa, walikuwa wakiteua Baraza la Mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi, wakuu wa mikoa wa wilaya nchi nzima.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia kutoka Chuo cha Diplomasia, Israel Sostenes, alisema alichokifanya Rais Magufuli ni kujaza nafasi muhimu kwa upande wa watendaji na watawala.
“Ameshateua Baraza la Mawaziri, wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa idara nyeti, hatua mbayo ni nzuri, wakuu wa wilaya siyo jambo la muhimu sana kwa sababu ameshapanga vyema safu yake ya ngazi ya juu,” alisema.
Alisema Rais Magufuli ana nia njema na ya dhati na kwamba anaangalia na kufuatilia kwa makini kabla ya kuteua ili kupata wanaotosha kwenye nafasi hizo.
Alisema kuchelewa kwa uteuzi huo, hakuwezi kutokana na kukosekana kwa fedha bali ni kuona namna anaweza kuokoa fedha kwa kuteua wakuu wa wilaya.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulhakim Atiki, alisema suala la kuteua wakuu kwa kujaza nafasi linatokana na Rais kuridhika na utendaji wa waliopo.
Alisema Baraza la Mawaziri ndiyo muhimu kwa sababu linavunjika, lakini kwa upande wa wakuu wa mikoa na wilaya wanaweza kuendelea kufanya kazi bila kuteua wapya.
“Huenda Rais ameona utendaji wao uko vizuri na akaishia kubadili wakuu wa mikoa pekee na wakuu wa wilaya akaendela kujaza nafasi. Hili ni jambo jema kwa sababu yuko makini na uteuzi wake,” alisema.
Naye Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda, alisema utaratibu huo alioufanya Rais Magufuli, ni jambo zuri kwani kitu cha msingi anachokiangalia ni utendaji wa kazi.
Alisema marais wanapoingia madarakani, wanakuwa na nafasi za uteuzi zaidi ya 5,000, hivyo Rais Magufuli anachokiangalia ni maslahi ya taifa na si vingine.
“Rais hajaingia kwa shinikizo la mtu ama kumchagua mtu kwa vile analipa fadhila, wapo wakuu wa wilaya ambao ni wazuri na amewabakiza hakuna umuhimu wa kuwaondoa wote, utaratibu mzuri ni kuangalia utendaji kazi kama ilivyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro alivyoachwa kulikuwa na sababu,” alisema Mbunda na kuongeza:
“Huu ni utaratibu mzuri wa utendaji kazi kwani anawafuatilia na baadaye kufanya uamuzi. Hii itasaidia kuongeza ufanisi wa kazi kwa viongozi wetu.
Imeandikwa na Mary Geofrey na Beatrice Shayo
Previous
Next Post »