Manispaa ya Kinondoni Dar inayoongozwa na CHADEMA, chini ya UKAWA imetangaza kila mwananchi wa Manispaa hiyo atachangia Shilingi 40,000 kwa mwaka ili aunganishwe na mpango wa matibabu wa Bima ya Afya Mpango huo utawawezesha kupata matibabu ya bure katika hospitali mbalimbali Mpango huo utaanza kutekelezwa mwezi Juni mwaka huu, huku bajeti ya Manispaa hiyo ikiongezeka kwa asilimia 59 kutokana na kukua kwa mapato ya ndani. Wazee wa Manispaa hiyo nao wametangaziwa neema ya matibabu bure kwani watapewa kadi maalum zitakazowawezesha kutibiwa hospitali za umma. Mapato hayo yametokana na ukusanyaji madhubuti katika kodi za majengo, mabango, leseni za biashara, huduma za kuegesha magari, hoteli na ruzuku ya serikali kuu. Bajeti ya mwaka 2016/2017 katika Manispaa hiyo inafikia Sh. Bilioni 248.47 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana ambayo ilikuwa ya Sh. Bilioni 156.24. Katika bajeti ya mwaka huu kuna ongezeko la Sh. zaidi ya bilioni 92. Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob aliwasilisha bajeti hiyo jana jijini Dar es Salaam katika kikao cha Baraza la Madiwani.
Sign up here with your email