TCCIA YAKIRI UBAGUZI KIBIASHARA EAC UMEPUNGUA. - Rhevan Media

TCCIA YAKIRI UBAGUZI KIBIASHARA EAC UMEPUNGUA.


CHAMA cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Dar es Salaam, kimesema changamoto za kubaguliwa katika nchi za Afrika Mashariki ambazo wanachama wake walikuwa wakikumbana nazo miaka ya nyuma zimeanza kupungua.

Hayo yalisemwa jana na Makamu Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Kingu Mtemi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake.
Alisema kulikuwapo na ubaguzi pale wajasiriamali wa Tanzania wanapopeleka bidhaa zao kuuza katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo na wakati mwingine kukataliwa zisipite, jambo ambalo lilikuwa ni kero kubwa kwao.
Alifafanua kuwa malengo makuu ya mtangamano wa jumuiya hiyo ni kukuza biashara, kuongeza ufanisi katika uzalishaji, kukuza uwekezaji wa ndani baina ya nchi wanachama na kuendeleza viwanda.
"Kwa sasa hali imekuwa shwari, zimebaki changamoto za kawaida tu ambazo hazina madhara kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wakati kukiwa na ubaguzi wa bidhaa zinazotoka Tanzania," alisema Dk. Mtemi.
Aidha, Dk. Mtemi pia alisema kuwa leo chama hicho kinatarajia kufanya uchaguzi huo leo ili kuwapata viongozi wapya watakakiongoza chama hicho katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Alisema kuwa katika uchaguzi huo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Charles Mwijage, ambaye amealikwa kushuhudia zoezi zima la kuwapata viongozi wapya wa TCCIA.
Alisema kabla ya uchaguzi huo watasoma na kuthibitisha muhtasari wa mkutano mkuu wa mwaka 2014, mahesabu yaliyokaguliwa ya mwaka 2015, mpango wa kazi na bajeti ya mwaka 2016, uteuzi na kuweka kiwango cha ukaguzi wa mahesabu ya mwaka 2016.
Previous
Next Post »