UKATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA WAGOMBEWA KWA NGUVU KUBWA. - Rhevan Media

UKATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA WAGOMBEWA KWA NGUVU KUBWA.



  Mgombea wa Nafasi ya  Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa, Bw. Igor Luksic ( Montenegro), akimwaga sera zake mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  wakati wa majadiliano/mhadalo  usio rasmi ulioandaliwa na  Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa lengo  kutoa fursa kwa wanaowania nafasi ya  Katibu mkuu kueleza sera zao na kisha kuulizwa maswali 
 Bi. Irina Bokova ( Burgalia) mmoja wa wanawake wanne waliojitokeza hadi sasa  kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa naye akijieleza mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 
Bw. Antonio Guterres ( Portugal) mmoja wa wagombea waliohojiwa  katika siku ya kwanza ya mdahalo  usio rasmi wa kuwasikiliza wagombea waliojitokeza kuwaania nafasi itakayoachwa wazi na Ban Ki Moon, mwishoni mwa mwaka  huu. jumla ya wagombe tisa wamekwisha jitokeza mpaka jana ( jumanne).
  Taswira ya  Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa,  katika siku ya kwanza ya mdahalo wa kihistoria ya wagombea  nafasi ya  Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mdahalo/majadiliano ya kwanza ya aina yake kufanyika katika   nafasi ya kumtafuta Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa .


Na Mwandishi Maalum, New York
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  jana ( Jumanne) limeandika historia kwa mara nyingine, kwa kuanza   mchakato usio  rasmi wa  kuwasikiliza na kuwauliza maswali  wagombea  watarajiwa waliojitokeza kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Mchakato huo ulianza kwa kuwasikiliza wagombea watatu kati ya tisa wakiwamo wanawake wake wanne  ambao hadi siku ya jumanne walikuwa wametangazwa rasmi kuwania nafasi hiyo itakayo achwa wazi na Katibu Mkuu wa  sasa   Ban Ki Moon anayemaliza muda  wake mwishoni mwa mwaka huu.

Katika awamu ya hiyo ya kwanza, kila  mgombea mtarajiwa  alipewa fursa ya kujieleza na kuelezea visheni yake,  sera, mipango, vipaumbele vyake  na nini anatarajia kukifanya  endapo  atachaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa  , Umoja  wenye wanachama 193.
Walioshiriki mdahalo huo katika siku ya kwanza  walikuwa ni  Dr. Igor Luksic ( Motenegro), Bi. Irina Bokova ( Bulgaria) na  Bw. Antonio Guterres ( Portugal)

Wengine ambao wamejitokea kuwania nafasi hiyo ni  Dr. Damilo Turk ( Slovenia) Prof.Dr. Vesna Pusic ( Crotia), Bi. Natalia Gherman ( Moldova), Dr. Srgian Kerim ( Macedonia),  Bi. Helen Clark ( New Zeland) na   Bw. Vuk Jeremic ( Serbia)

Ulikuwa ni mdahalo wa aina yake wa kwanza kutokea tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa miaka karibu  70  iliyopita, mdahalo  ulioendedeshwa katika  mazingira ya uwazi, na ambao kwayo umebadilisha kabisa utaratibu wa kumpata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Previous
Next Post »